NA MWANDISHI WETU
JUMUIYA ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wake Hadija Ally imekamilisha safu zote za uongozi huku ikitoa dira yenye kutekeleza mambo matano yenye maslahi kwa Watanzania wote.
Akizungumza leo katika Ukumbi wa Karimjee Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Dar es Salaam, Hadija Ally, amesema ameitisha Baraza lake rasmi la mkoa ambapo wameteua wajumbe wa baraza pamoja na wajumbe wa kamati ya utekelezaji kwa ridhaa ya wajumbe wa baraza wa mkoa huo.
“Sasa safu ya jumuiya ya wazazi Mkoa wa Dar es salaam imekamilika ina wajumbe wa utekelezaji, wajumbe wa kamati tendaji lakini pia tuna wajumbe wa baraza rasmi na hii leo tumefanya baraza letu la kwanza.Nitoe dira ya Jumuiya ya wazazi Mkoa huu.
“Tunakwenda kusimama katika mambo matano na haswa suala zima la elimu, malezi ,mazingira , afya na uchumi ndani ya Dar es Salaam. Jumuiya ya wazazi ni jumuiya pekekee inayohusika na kazi hizo tano .Jumuiya pekee ambayo inahusika na masuala haya ndani ya chama na nje ya Chama kwa maana ya jamii yetu kwa ujumla hata kama sio mwanachama wa jumuiya yetu ya wazazi lakini mambo inayoyatekeleza yana faida kwa watu wote wote,”amesema Hadija Ally.
Aidha amesema kazi ya kwanza ni kuhakikisha elimu na mazingira, elimu na malezi, elimu na maadili inasimamiwa vema lakini pia mmomonyoko wa maadili umekithiri ndani ya Mkoa wetu wa Dar es Salaam hivyo jumuiya kwa kushirikiana na makatibu wao wa kata zote 102 wanakwenda kusimamia hayo kwa kuweka mikakati.
Miongoni mwa mikakati hiyo kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo wataanzisha mafunzo ya uongozi kupitia kamati ya utekelezaji na kupitia kamati za wilaya.
“Tutatoa mafunzo ya uongozi, kwanza tuwe na viongozi wenye maadili lakini pia kutoa mafunzo ya kupinga unyanyasaji wa kijinsia na ukatili uliokuwepo kwa watoto wetu na wanawake. Kwa hiyo niseme dira ya jumuiya ya wazazi Mkoa wa Dar es salaam tutapambana na maadili na kwa pamoja tutashirikiana na serikali.
“Ndio kazi iliyokuwepo ya Chama na Jumuiya zake kushirikiana na serikali kuhakikisha lile ambalo linakusudiwa kwenye jamii husika linafanyika.Pia jumuiya ya wazazi inakwenda kuandaa mpango kazi wa miaka mitano kwa ajili ya kutekeleza maeneo matano tuliyoainisha kwa kushirikiana na kamati za utekelezaji na kushirikiana na wilaya.”
Amesema lengo ni kuhakikisha ndani ya miaka mitano hadhi na heshima ya jumuiya ya wazazi inaruddi lakini pili wanatenda kazi iliyotukuka kuhakikisha Serikali yao na Chama chao mwaka 2024/2025 wanapata ushindi wa kishindo kwasababu watakuwa wametenda kazi.
Ameihakikishia Dar es Salaam kuwa Jumuiya ya Wazazi iko salama kwasababu wanakwenda kuyasimamia mambo matano ya jumuiya hiyo na dira ya miaka ya mitano itaonekana .“Narudia tena kuwapongeza walioshinda nafasi ya wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji Mkoa wa Dar es salaam na walioshinda kuingia Baraza la Mkoa.”
No comments:
Post a Comment