TFRA YAWATAKA WADAU WA MBOLEA KUZINGATIA SHERIA - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Tuesday, July 11, 2023

TFRA YAWATAKA WADAU WA MBOLEA KUZINGATIA SHERIA

Mkuu wa Mkoa wa Dar es  Salaam Mhe. Albert Chalamila  akipokea zawadi  kutoka kwa watumishi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania alipotembelea banda la Mamlaka leo tarehe 11.07.2023  kwenye viwanja vya  maonesho ya  Sabasaba yanayoendelea  jijini  Dar es Salaam

  Mteknolojia wa Maabara wa  Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)  Bw.Yohana Masalapilu akitoa elimu kuhusu majukumu ya Mamlaka kwa wadau wa mbolea waliotembelea banda la TFRS wakati wa Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa  Sabasaba  yanayoendelea jijiini  Dar es Salaam.


Ofisa Udhibiti Ubora wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Peter Mwanguku akijibu maswali ya mdau aliyetembelea banda la Mamlaka wakati wa Maonesho ya Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam.

NA MWANDISHI WETU

MAMLAKA ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA),kupitia kitengo chake cha Sheria kimetoa wito kwa wakulima, wafanyabiashara na wazalishaji wa mbolea nchini, kufuata utaratibu wa sheria katika kutimiza majukumu yao ili kusaidia kuepuka kuingia kwenye migogoro na Serikali.

 Wito huo umetolewa jana na Mwanasheria wa TFRA, Godfrey Munisi  katika viwanja vya Maonesho ya 47 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) jijini Dar es Salaam ambayo yamepangwa kufikia tamati Julai 13 mwaka huu.

Munisi ameongeza kuwa Serikali iko macho katika kuhakikisha mbolea inayomfikia mkulima inakuwa na viwango vinavyokubalika ili kuchochea maendelea chanya katika sekta ya kilimo nchini jambo litakalosaidia kuendelea kuinua uchumi wa taifa.

“Katika kuhakikisha mkulima anapata mbolea sahihi katika matumizi yake, Serikali inafanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa wafanyabiashara ili kutambua mbolea iliyosajiliwa ndio inayouzwa au la, pia wanafanya uchambuzi wa kimaabara ili kubaini ubora wake wa virutubisho vinavyohitajika kabla ya kumfikia mkulima,” amesema.

Amesema wanafanya uchambuzi wa kimaabara kwa mbolea zinazozalishwa ndani na zile zinazoingizwa kutoka nje ya nchi ili kuweka usalama kwa taifa kupitia kilimo na wanapojiridhisha ndipo wanaruhusu ziende kwa wafanyabiashara na baadaye kumfikia mkulima ambaye anapata mbolea stahiki.

Pia ameweka wazi kuwa jambo lingine ambalo TFRA, inafanya ni kutoa elimu kwa mkulima kuhusu matumizi sahihi ya mbolea itakayowasaidia kutimiza malengo yao katika nyanja ya kilimo ambayo wameamua ndio iwe sehemu ya kuendesha maisha yao.

Mwanasheria huyo wa TFRA, ameongeza kwamba licha ya kuhakikisha mbolea inayozalishwa na inayoingizwa nchini inakuwa salama na bora kwa matumizi ya shambani  jambo kubwa ambalo wanashughulika nalo ni kutoa leseni na vibari kwa wafanyabiashara wa mbolea.

Naye, Kaimu Meneja TEHAMA katika Mamlaka hiyo, Salehe Kejo amebainisha kuwa katika kutoa huduma kwa wadau wa sekta hiyo wanatumia mifumo mbalimbali ukiwamo wa kidigitali (On Line) unaosaidia wafanyabiashara wa mbolea kujisajili na kujaza fomu ya kuomba leseni.

Ameongeza kuwa baada ya kukamilisha mchakato wa kuomba leseni kupitia tovuti ya TFRA , mfanyabiashara ataweza kupata huduma ya kusajili mbolea inayotoka nje ya nchi na pindi taratibu zitakapokamilika ataruhusiwa kuuza mbolea yake hapa nchini.

Pia kupitia tovuti hiyo mfanyabiashara anaweza kuomba kibari cha kuingiza mbolea kutoka nje ya nchi, njia ambayo  ni rahisi kwa wadau wa sekta hiyo hiyo kuifuata na kukamilisha mahitaji yao kwa kipindi kifupi.

Kejo, ameongeza kuwa mfumo mwingine wa kidigitali ambao wanahusika nao ni wa ruzuku ya mbolea unaotumika kusajili wakulima, wafanyabiashara  walio katika mpango huo na kusajili mbolea zilizo katika mpango wa ruzuku.

“Katika mfumo wa kusajili mbolea unapokamilika, tunaweka bei elekezi katika mifuko inayowekewa mbolea na mkulima husika anapata fursa ya kulipa kiasi kilichopangwa na kilichobaki kinalipwa na Serikali ikiwa ni sehemu ya ruzuku.

“Ili kukamilisha mchakato huo mfanyabiashara atatakiwa kujisajili katika App ya TFRA ambayo itamuunganisha  na mfumo wa ruzuku na kumpa bei elekezi iliyopangwa na Serikali, hivyo mkulima ili kupata mbolea ya ruzuku atafika na namba yake iliyosajiliwa,” amesema.

Ameongeza kuwa Mamlaka hiyo inatumia mfumo huo ili kutekeleza majuku yake kwa haraka, pia inatoa taarifa zake kupitia tovuti ya tfra.go.tz zikiwamo za mbolea zilizosajiliwa, bei elekezi na habari nyinginezo kuhusu mbolea.

No comments:

Post a Comment