NA MASHAKA MHANDO, KOREGWE
CHAMA cha Mapinduzi (CCM)
mkoa wa Tanga, kimetoa maelekezo kwa Mkuu wa Wilaya Korogwe Jokate Mwegelo
kupitia Katibu Tawala wake (DAS) Mwanaid Rajabu, wahakikishe vituo vya afya vya
Kerenge na Mnyuzi vinamalizika haraka ili vianze kutoa matibabu kwa wananchi.
Akizungumza katika siku
yake ya kwanza katika mwendelezo wa ziara zake kukagua uhai wa chama na
utekelezaji wa ilani ya chama, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tanga Rajabu Abdallah
ambaye alitoa maelekezo hayo baada ya kutofurahishwa na kasi ndogo ya utekelezaji
wa miradi hiyo.
Aidha aliiomba Ofisi hiyo ya DC kufuatilia kwa makini taarifa za kibank
ili kuweza kujiridhisha na matuminzi ya fedha za miradi hiyo baada ya
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Korogwe Vijijini kueleza kwamba kipo
kiasi cha fedha kimebaki ingawa mradi huo umesimama kwa sasa.
Rajabu alisema Serikali
imetoa kiasi cha shilingi bilioni 1 kwa ajili ya ujenzi wa vituo hivyo vya afya
kwa lengo la kuwasaidia wananchi wanaoteseka kwa kutembea umbali mrefu zaidi ya
km 40 kufuata huduma Korogwe Mjini jambo ambalo ni hatari kwa maisha ya
wananchi hao.
"Mna DC makini sana
katika wilaya hii na naomba nitoe maelekezo yafuatayo, DAS hakikasha unamwambia
DC mfuatilie majengo haya na yaishe mapema wananchi wetu wapate huduma, lakini
pia fatilieni fedha kama ipo kweli kwenye akaunti" alisema na kuongeza,
"Haiwezekani Rais Dkt Samia Suluhu Hassan atafute fedha kwa
kuzunguka huko na huko halafu watu washindwe kuzisimamia, watumishi mliopewa
dhamana fanyeni kazi kwa weledi wenu na maelekezo haya tunayoyatoa kama
hamtayafanyia kazi mtajua chama hiki ni kikubwa kuliko mtu yeyote yule,".
Alisema kinachofanywa na watendaji na Viongozi Wilayani hapo kwa
kutokukamilisha ujenzi wa vituo hivyo ni kumchonganisha Rais, Mbunge na hata
Diwani dhidi ya wananchi na kuonekana Serikali haiwajali wananchi wake kumbe
Korogwe wameletewa fedha nyingi katika miradi mbalimbali lakini watendaji
wanashindwa kuzisimamia.
Alisema vipo vituo vya afya vimejengwa kwa gharama hizo hizo za Shs Mil
400 karibu Mkoa mzima wa Tanga na majengo yote yamejengwa tofauti na Korogwe
ambapo wamepokea shs Mil 500 kwa kituo kimoja na havijakamilika hali
inayoonekana kuna matuminzi mabaya ya fedha.
Aidha alisema pesa nyingi zimeelekezwa Wilayani Korogwe kwa ajili ya
miradi ya vituo vya afya jambo la kusikitisha vituo hivyo havijakamilika na ni
dalili za wazi zinazoonyesha Wilaya ya korogwe imeonyesha kiasi gani kuna
uzembe wa usimamiaji wa miradi ya maendeleo.
Rajabu aliwataka viongozi
waliopewa dhama na Rais wafanye kazi kwa weledi na watambue kufanya hivyo
kutasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa kama sio kumaliza kero za wananchi hasa
katika miradi ya kimaendeleo.
Kwa upande wake Mbunge wa Korogwe Vijijini Timotheo Mzava alisema kwanza
wanamshukuru Mh, Rais kwa kutoa Bil 1 kwa ajili ya ujenzi wa vituo viwili vya
afya ambapo Kituo cha afya cha Kerenge Shs Mil 500 na kile cha Mnyuzi Shs Mil
500 na kushukuru maelekezo ya Mwenyekiti huyo kwamba yatasaidia wananchi.
Aidha alisema changamoto ya utekekezaji wa miradi hiyo ni ucheleweshwaji
na hata majengo yaliyokuwatayari hayakuanza kutumika ingawa uhitaji wa huduma
hiyo ni mkubwa kwa wananchi wa maeneo hayo.
Alitumia fursa hiyo kuiomba Serikali ijitoe kwa nguvu zote ili
utekelezaji wa vituo hivyo vya afya vikamilike kwa wakati ili kuwaondolea adha
wananchi hao kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya afya.
Akitoa taarifa fupi ya mradi huo Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya
Korogwe Halfan Magani alisema miradi hiyo imechelewa kutokana na taratibu za
kimanunuzi kupitia mfumo wa force Account kupitia kamati ambazo zipo Kijijini.
Alisema mbali ya changamoto hiyo ya mfumo wa kimanunuzi pia
mkandarasi alishindwa kuendelea na mradi na Halmashauri ipo kwenye mchakato wa
kumtafuta mkandarasi mwengine ili aweze kumalizia sehemu iliyobaki.






No comments:
Post a Comment