
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk. Moses Kusiluka (kushoto)
akipokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Saddy Kambona
(kulia) katika banda la bodi hiyo kwenye Maonesho ya Nanenane jijini Mbeya
alipotembelea banda hilo jana. Katikati ni Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na
Uvuvi, Profesa Riziki Shemdoe.
NA MWANDISHI WETU, MBEYA
MKURUGENZI Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Saddy
Kambona amebainisha moja ya malengo ya bodi hiyo kwa mwaka huu 2023 ni
kuzalisha tani 60,000 kutoka tani 48,000 mwaka 2022.
Kambona amesema hayo jijini Mbeya katika Maonesho
ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya John Mwakangale.
Amesema mwaka 2020 wakati TSB inapewa jukumu na
serikali la kuhakikisha uzalishaji unapanda hadi kufikia tani 120,000 mwaka
2025, ilikuwa inazalisha tani 36,000 kwa mwaka na sasa hivi wamefunga mwaka
2022 kwa kuzalisha tani 48,000.
"Lengo letu ni kufikisha tani 60,000 na
tayari hadi kufikia Juni mwaka huu tulikuwa tumeshazalisha tani 34,000. Kwa
hiyo tunajiona kabisa tutamaliza mwaka 2023 kwa kuzalisha tani 60,000 bila
wasiwasi.
"Jitihada zimeshafanyika ambapo serikali
imeongeza bajeti ya maendeleo ya Bodi ya Mkonge kwa kuiwezesha kupata vyombo
vya usafiri kwa ajili ya kushughulikia upatikanaji wa takwimu ambao ulikuwa
changamoto ndiyo maana utaona sasa hivi takwimu zimepanda siyo kwamba Mkonge
haukuwepo lakini takwimu zilikuwa hazikusanywi ipasavyo, kimsingi mabadiliko ni
makubwa," amesema.
Akizungumzia takwimu za mapato Kambona amesema
tangu serikali imechukua juhudi za kufufua zao la Mkonge mwaka 2019 na
kutambulishwa kuwa zao la kimkakati mapato ambapo mauzo ya nje yameongezeka
ambapo kwa mauzo ya nje pekee yamefikia Dola za Marekani milioni 56
kutoka Dola milioni 42 kwa kipindi cha miaka miwili.
"Lakini mauzo ya ndani pia yaliongezeka kutoka
Sh bilioni 41 hadi sasa Sh bilioni 43 kwa soko la ndani. Kwa hiyo soko la nje
limefanya vizuri zaidi yaani Mkonge mwingi umeuzwa zaidi nje kuliko ndani
lakini mwisho wa siku takwimu zimepanda," amesema Kambona.
Pamoja na mambo mengine, amesema wastani wa mauzo
ya singa za Mkonge (fiber) tani moja ni takribani Sh 3,500,000 kwa madaraja ya
juu.




No comments:
Post a Comment