Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya kukagua maendeleo ya Ujenzi wa Barabara ya Mabasi yaendayo Haraka BRT awamu ya tatu inayoanzia eneo la Posta ya Zamani – Gongolamboto leo jijini Dar es Salaam.
NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa
ameuagiza Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kuanzia sasa kutowapa
kazi wakandarasi wote wanaochelewesha miradi ya ujenzi na menejimenti
zao kufikishwa ofisini kwake mara moja kwa hatua zaidi.
Amewataka wasimamizi wa miradi ya barabara kuwa wabunifu na kusimamia majukumu yao kikamilifu ili kuondoa changamoto ndogondogo kwa watumiaji wa miundombinu ya ujenzi wa barabara nchini.
Bashungwa amesema hayo jijini Dar es Salaam, wakati wa ziara yake ya kukagua athari za mvua, mradi wa mabasi yaendayo kasi awamu ya tatu na miradi mingine ya ujenzi inayoendelea jijini Dar es Salaam.
Amewaagiza Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kuanzia sasa mradi wowote wa barabara unaojengwa nchini katika hatua ya usanifu lazima washirikiane na taasisi zingine za Serikali ili kuondoa matatizo ya kiutendaji pale ambapo mradi unakamilika na taasisi nyingine inataka kutekeleza mradi wake eneo hilo.
Amesema atakuwa mkali kwa watendaji au wakandarasi wazembe wanaoshindwa kwenda na kasi ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kusababisha miradi kusuasua.
Ameonya tabia ya baadhi ya wakandarasi kujenga miradi mingi kwa wakati mmoja na yote kutokuwa kwenye kasi inayotakiwa kimkataba.
"..Serikali inapotia fedha inahitaji huduma kwa haraka hivyo mameneja nchini kote hakikisheni miradi inakamilika kwa wakati", amesisitiza Waziri Bashungwa.
Aidha amekemea tabia ya baadhi ya wananchi kuvamia hifadhi za barabara kinyume cha sheria na kufanya biashara hali inayosababisha usumbufu na usalama hafifu kwa watumiaji wa barabara.
Aliongeza, "hifadhi ya barabara iko kwenye sheria tangu mwaka 1932 hivyo TANROADS na TARURA isimamieni kikamilifu sheria hiyo", amesisitiza Bashungwa.
Ametoa wito kwa wakandarasi wazawa kufanya kazi kwa bidii ili kuleta tija na kuliwezesha Serikali kuwaamini na kuwapa miradi mingi ili kukuza uchumi wa watanzania.
Ameitaka bodi ya ushauri ya Tanroads kukutana mara moja ili kuidhinisha ujenzi wa miradi mipya ya barabara.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa TANROADS Eng. Dorothy Mtenga amesema ujenzi wa BRT III unaotekelezwa na Mkandarasi Sinohydro unatarajia kukamilila mwezi Machi 2024.
"Tumepokea maelekezo yote yaliyotolewa na Serikali tutaendelea kumsimamia mkandarasi kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa kama Serikali inavyotaka katika mradi huo wa BRT awamu ya tatu.
Alikiri kuwa ujenzi wa mradi huo upo nyuma kimkataba ambapo sasa uko asilimia 20 wakati ulitakiwa kuwa asilimia 46.
Meneja Mradi wa Kampuni ya Sinohydro, Guo Kun aliahidi kumaliza ujenzi kwa wakati kwani watakuwa wanafanyakazi usiku na mchana.
Kuhusu kupunguza changamoto kwa wananchi wakati wa ujenzi wa mradi huo alieleza kuwa mkakati wa kampuni yake ni kujenga zaidi usiku kuliko mchana.
No comments:
Post a Comment