HATUWAHITAJI VIONGOZI WASIO WAJIBIKA KWA WANANCHI - GAVU - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Sunday, November 26, 2023

HATUWAHITAJI VIONGOZI WASIO WAJIBIKA KWA WANANCHI - GAVU

                                                                    


NA MWANDISHI WETU

KATIBU wa NEC,Organaizesheni Taifa, Issa Haji Ussi Gavu amesema kiongozi yeyote ambaye amepewa dhamana na wananchi akashindwa kuwatumikia huyo hafai kurudi tena 2024 na amesisitiza wasipewe nafasi za kuongoza ndani ya CCM kwa kutowatendea haki wanaowaongoza.

Gavu ameyasema hayo wakati akiwahutubia Wazee wa CCM Mkoa wa Pwani kwenye mkutano  uliofanyika Picha ya Ndege Kibaha mkoani humo.

"Tumepata taarifa wapo baadhi ya wenyeviti wetu wa vijiji, vitongoji na mitaa wanashindwa kukidhi matakwa ya katiba na kanuni, yaani viongozi wasiowajibika kwa wananchi hivyo mwakani wasipewe nafasi" amesema Gavu.

"Kama wenyeviti wetu wanashindwa kuitisha vikao wala mikutano ya kuelezea mapato na matumizi ya achaneni nao, badala yake tafuteni wenyeviti wa vijiji, mitaa au vitongoji wanaokubalika mbele za wananchi" amesema Gavu.

Amefafanua kuwa hakuna sababu ya kupanda mlima wakati kichuguu kipo, huku akiwahimiza kutafuta  watu wanaouzika ambao watakisaidia chama na kuhangaika na mambo ya watu wanaowaongoza"

Ameongeza kuwa ziko taarifa kwamba baadhi ya wabunge, madiwani wanahangaika kupanga safu za viongozi wa vitongoji, vijiji na mitaa kwa madhumuni ya kwamba wawasaidie kwenye kura za maoni ifikapo uchaguzi Mkuu 2025.

"Tunamuhitaji diwani, mbunge apambane ili wenyeviti wa vijiji, vitongoji na mitaa ndani ya kata yake na ndani jimbo lake washinde kwa kura za walio wengi na ikitokea mbunge au diwani amepoteza mitaa, vijiji, vitongoji kwenye eneo lake basi na yeye atakuwa kwenye wakati mgumu wa kupoteza nafasi yake ya kugombea tena" amesema Gavu.

Gavu amesema viongozi walioko madarakani ndio daraja baina yao na watu wanaowaongoza, kama daraja likivunjika basi hakuna namna ya kufika ng'ambo ya pili.

Aidha amewataka viongozi wa CCM na wanaccm kufanya vikao vya kikatiba ili kujua kero na changamoto zinazowakabili wananchi wanaowaongoza na kuzitafutia ufumbuzi.

Amesema kumekuwa na tatizo kubwa la viongozi kutotimiza wajibu wa kukaa vikao vya kikatiba na vya kikanuni ndani ya CCM.

Amesema kwa mujibu wa ibada 124 ya Katiba ya CCM, Wazee ni taasisi na wanatakiwa kuhudhuria vikao halali vya chama. 

"Rudini mkasome kanuni toleo la mwaka 2019 kuanzia ibara ya tatu ambayo inaelezea madhumuni na umuhimu wa kuanzishwa kwa Baraza la Wazee ni kurithisha tabia njema kwa taifa letu" amesema.

Amesema Baraza la Wazee ni chombo cha kuwaunganisha wazee wote kwa itikadi ya CCM na  kuwasihi wasione tabu wala shida kurudi kwenye ngazi husika ya wilaya, kata, au tawi kwa ajili ya kutoa ushauri ili mambo yaende vizuri.

"Mkichelea kusema au kushauri mtakuwa hamkitendei haki chama chetu, taifa na hamuitendei haki nafasi na fursa mliyopewa na katiba yetu maana ninyi ni washauri mambo yakienda vibaya hamna namna ya kukataa lawama hizo, mtabeba msalaba huo wa kutokushauri, kutoongoza na kutokutupa maelekezo ili mambo yanyooke" amesema Gavu.

Amehitimisha kwa kusema, CCM ni chama cha watanzania wa tabaka zote awe mnyonge au tajiri, awe mrefu au mfupi, awe mweupe au mweusi mategemeo yake na kimbilio lake ndani ya taifa hili ni CCM tu.





No comments:

Post a Comment