KATIKA KUADHIMISHA SIKU YA KISUKARI DUNIANI, FAHAMU KIASI CHA SUKARI KILICHOPO MWILINI KWA KIPINDI CHA MIEZI MITATU - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Monday, November 13, 2023

KATIKA KUADHIMISHA SIKU YA KISUKARI DUNIANI, FAHAMU KIASI CHA SUKARI KILICHOPO MWILINI KWA KIPINDI CHA MIEZI MITATU

          Mtaalamu wa maabara katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke, Maryam Karume.

                                                ................................................................

UGONJWA wa kisukari ni moja ya magonjwa yanayoweza kuhatarisha maisha yetu ya kila siku  katika jamii. Kupanda na kushuka kwa viwango vya sukari mwilini kunaweza kuwa hatari isiyotambulika mara moja, na ndio maana kupima sukari mara kwa mara ni muhimu zaidi kuliko hapo awali. 

Kwa kutambua hilo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke inakipimo maalumu cha kupima sukari kwa wagonjwa wa kisukari na wale wanaohitaji kufuatilia viwango vyao vya sukari mwilini kwa kipindi cha muda mrefu. 

Kipimo hicho ni HbA1c. HbA1c si tu kipimo cha kawaida cha sukari mwilini; ni zaidi ya hayo. Kipimo hiki kina uwezo wa kuchunguza kiasi cha sukari kilichopo ndani ya mwili wa mgonjwa kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita. Hii ina maana kwamba, badala ya kupata picha moja tu ya kiasi cha sukari mwilini kwa wakati huo, HB1c inatoa mwangaza kwa jinsi mwili wa mgonjwa unavyoshughulikia sukari kwa muda mrefu.

Kipimo cha HbA1c ni tofauti na vipimo vingine vya sukari ambavyo mara nyingi huhitaji mtu kuwa njaa yani kutokula chakula chochote. Mtaalamu wa maabara katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke, Maryam Karume, anaelezea kwamba HbA1c ina uwezo wa kutambua kiwango cha sukari kilichokuwepo mwilini kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita.

“Jambo kubwa la kuvutia kuhusu HbA1c ni kwamba inaweza kutoa picha kamili ya jinsi mwili unavyoshughulikia sukari kwa muda mrefu zaidi”. Hii ni muhimu sana katika kudhibiti na kuzuia magonjwa ya kisukari. 

Ameongeza kwa kuasa  wananchi kujenga tabia ya kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara kwani Kupitia kipimo hiki cha HbA1c, tunaweza kugundua mapema mienendo ya sukari mwilini na kuchukua hatua kabla hali haijawa mbaya zaidi.

Kwa kuweka afya yetu mikononi mwetu na kufuata ushauri wa wataalamu wa afya, tunaweza kudhibiti ugonjwa huu hatari na kujenga mustakabali wenye afya kwa kila mmoja wetu. Kupitia kipimo hiki, tuna njia imara ya kusimamia afya zetu na kuishi maisha yenye furaha.




No comments:

Post a Comment