Waziri wa Sheria na Katiba wa Uganda ,Nobert Mao (kulia) wakijadiliana jambo na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA),Godfrey Nyaisa (katikati) huku Msajili Mkuu kutoka Taasisi ya Usajili Uganda, Mercy Kainobwisho (kushoto) akifuatilia, wakati wa Mkutano wa 19 wa Baraza la Mawaziri wa nchi wanachama wa ARIPO unaofanyika Gaborone, Botswana.
NA MWANDISHI WETU
RAIS wa Botswana, Dkt Mokgweetsi Eric Masisi amewataka mawaziri kutoka nchi wanachama wa Shirika la Miliki Ubunifu Kanda ya Afrika (ARIPO) kuhakikisha wanaongeza nguvu kwenye Miliki Ubunifu badala ya kutegemea Rasilimali pekee.
Kiongozi huyo ametoa rai hiyo leo Novemba 24, 2023 wakati akifungua Mkutano wa 19 wa Baraza la Mawaziri wa nchi wanachama wa ARIPO unaofanyika Gaborone, Botswana.
Amesisitiza kuwa muda umefika kwa nchi za Afrika kuwekeza kwenye maarifa na ubunifu na siyo kutegemea rasilimali tu na kutolea mfano katika kipindi cha Uviko 19 nchi za Afrika zilikuja na bunifu nyingi zikiwa ni pamoja na dawa na vifaa kinga, hivyo bunifu kama hizo zinapaswa kuendelea.
Pia amewataka mawaziri kuongeza bajeti zao kwenye masuala ya Miliki Ubunifu, katika mkutano huo Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Godfrey Nyaisa amemwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji.
Mkutano huo pamoja na mambo mengine umemchagua, Mmusi Kgafela, Waziri wa Biashara na Viwanda wa Botswana kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa ARIPO kwa kipindi cha miaka miwili.
Mkutano huo wa siku mbili wa Baraza la Mawaziri hufanyika kila baada ya miaka miwili na mkutano uliopita wa mwaka 2021 ulifanyika, Victoria Fall Zimbabwe.





No comments:
Post a Comment