SALMA MADAI IT ANAYETEMBEA NA NDOTO ZA RAIS DKT SAMIA - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Saturday, November 25, 2023

SALMA MADAI IT ANAYETEMBEA NA NDOTO ZA RAIS DKT SAMIA

                       

NA SELEMANI MSUYA

WANAWAKE ni moja ya kundi ambalo linatajwa kuwa na ushiriki mdogo katika siasa, hasa katika nchi maskini, ikiwemo Tanzania.

Kwa miaka ya karibuni kumekuwepo na mwamko wa kundi hilo kujitokeza kushiriki siasa, hali ambayo imeshuhudia wanawake wakigombea nafasi ya urais, ubunge, udiwani, uenyekiti wa Serikali za mitaa na hata ndani ya vyama vya siasa.

Kwa Tanzania inasemekana uwiano wa wanawake katika uongozi wa kisiasa bado ni chini ya asilimia 30, hivyo juhudi zimekuwepo kuhakikisha lengo la 50 kwa 50 linafikiwa kama dunia inavyotaka.

Lengo hilo limekuwa likisukumwa na ufanisi wa uongozi wa wanawake katika nafasi ambazo wanazopata, hali ambayo kila kukicha jamii imeendelea kuamini kundi hilo na kulipa nafasi ya kuwavusha.

                    

Kwa Tanzania  tuna ushahidi  wa kutosha, kwani tuna Rais mwanamke ambaye awali alikuwa mwaharakati, mbunge, waziri, makamu wa rais na sasa ni rais ambaye kwa miaka miwili na nusu ameonesha wanawake wanaweza.

Huyo sio mwingine ni Rais na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, mtoto  aliyezaliwa Kijiji cha Kizimkazi, Unguja Zanzibar.

Mwana mama huyo ambaye anatoka katika familia ya kawaida alipata nafasi ya Urais baada ya mtangulizi wake, Hayati John Magufuli kufariki na Katiba ya Tanzania imeweka bayana ni nani anapaswa kuchukua nafasi hiyo baada ya tukio kama hilo kutokea.

Rais Samia ndani ya miaka miwili na nusu ameonesha anaweza jambo ambalo linatoa majibu kuwa wanawake wanaweza na sio lazima kuwezeshwa.

Pia tuna Spika wa Bunge mwanamke Dk Tulia Ackson ambaye kusema kweli ameonesha uwezo wa wanawake kuongoza na hali hiyo imepelekea Oktoba 2023 achaguliwe  kuwa Spika wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU).

Pia wapo wanawake wengine kama Halima Mdee, Ester Matiko, Ummy Mwalimu, Profesa Joyce Ndalichako na wengine ambao wamekuwa wapambanaji sahihi katika siasa za Tanzania na wamefaulu.

     

Ok makala hii haikulenga kuwaelezea wakina mama hao ambao kisiasa wamefanikiwa bali ina muhusu msichana ambaye anatamani kuwa kama hao, naye si mwingine ni Salma Ramadhani Madai maarufu kwa jina la Salma wa Samia Suluhu.

Salma ni moja ya wakina dada shupavu na mpambanaji mwenye asili ya Wilaya ya Manyoni mkoani Singida anasema, Rais Samia amekuwa kiigizo chema kwenye harakati zake za kisiasa.

Anakiri kuwa pia wapo wanaume kama Rais mstaafu Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu mstaafu Fredrick Sumaye na Edward Lowassa ambao kwa miaka mingi amekuwa akiwafuatilia na anaamini katika kundi hilo ndipo Salma wa Samia anaonekana leo kama moja ya wanasiasa ambao wanafanya viziru.

Salma ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake (UWT) Tawi la Mbezi Luis na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam anasema amepata nafasi hiyo kutokana na kujituma na kwamba lengo lake ni kuwa kiongozi mkubwa zaidi.

“Mama Samia ni kiigizo chema kwangu, hivyo kila ninachofanya katika siasa na shughuli zangu zingine ni katika kutembea kwenye hatua za Rais Samia na hii imenivutia mimi kujiita Salma wa Samia Suhulu. Naamini ipo siku nitafika huko alipofikia Rais wangu kipenzi,” anasema.

                                   

Mwanadada huyo anasema ndoto yake ni siku moja awe diwani, mbunge au rais hali ambayo itamuwezesha kufikia kundi kubwa la wananchi, ili aweze kutoa msaada.

Anasema amekuwa akisaidia jamii inayomzunguka kupitia taasisi yake ya DMI Foundation, hivyo kupitia udiwani ataweza kufikia kundi kubwa zaidi.

“Mimi napenda kusaidia jamii, hivyo nikipata nafasi ya kuwa diwani, mbunge au rais naamini nitagusa kundi kubwa zaidi ya ilivyo sasa, lakini pia naona natosha kwa nafasi hiyo kwa sasa, ila ndoto yangu ni siku moja niwe mbunge hadi kufikia urais mbona Samia ameweza kwanini mimi nisiwe na ndoto hiyo,:” anasema.

Anasema siasa ni nzuri kama utafuata misingi yake na iwapo utafanya kinyume unaweza kuona siasa ni mchezo mchafu, jambo ambalo sio kweli.

“Siasa ni pesa, ili kushiriki siasa lazima ujiandae, hili haliepukiki, kinyume na hapo mwanamke unaweza kutumika bila matakwa yao. Lazima tujiandae kama tunataka kushiriki siasa za uongozi,” anasema.

Salma wa Samia anasema iwapo wasichana na wanawake watajiamini hakuna ambacho kinashindikana kwenye siasa kwani Rais Samia, Spika wa Bunge Dk Tulia na wengine wameonesha inawezekana.

Salma anasema katika maisha yake anaamini katika kujaribu na kujifunza na kwamba ameshiriki siasa na kwa sasa anaelewa changamoto zake, hivyo anajua njia gani za kupita kufikia mafanikio zaidi.

Mwanasiasa huyo ambaye kitaaluma ni Mtaalam wa Teknolojia ya Habari (IT) anasema jamii inapaswa kumuunga mkono Rais Samia kwani mambo ambayo anayafanya kwa ajili ya nchi yanaonekana.

Anasema yeye haamini katika majungu na maneno, bali vitendo na hicho ndicho kinafanywa na Rais Samia katika uongozi wake, huku akiweka bayana kuwa anaiona Tanzania mpya siku zijazo.

Salma anasema alipata elimu ya Shule ya Msingi Utemini kuanzia mwaka 1992 hadi 1998 na Sekondari ya Salmin Amour 1999 hadi 2002.

Kada huyo wa CCM anasema taaluma yake ya IT hajaitumikia kwa muda mrefu, kwani ndoto yake ilikuwa ni kufanya biashara na shughuli za kijamii.

Anasema amefanya biashara ya kuuza viatu na nguo kwa takribani miaka 12 na baadae aliamua kujikita katika siasa ambayo anafanya hadi sasa kupitia CCM.

                             

Anasema baadae aliamua kubadilisha biashara ya nguo na viatu, ambapo alianza kuuza virutubisho vya tiba lishe na duka moja la nguo kwa njia ya mtandaoni na kwamba anakiri kupata mafanikio makubwa.

“Biashara hii ya virutubisho vya tiba lishe nauza Tanzania, Rwanda, Burundi, Uganda, Kenya, Zambia na kwingineko ambapo anakira kuwa elimu yake ya IT imekuwa msaada kwake zaidi.

Anasema anatumia mawakala na teknolojia za mitandaoni zimekuwa chachu ya yeye kufanikiwa katika biashara hiyo ambayo anazalisha bidhaa zote kwa kutumia kiwanda kidogo anachomiliki.

“Katika maisha kila ulichosomea sio unachokifanyia kazi, hivyo baada ya kuona kuna changamoto ya maradhi, niliamua kutumia taaluma yangu ya IT kusaidia kundi kubwa la binadamu wenzangu. Lakini kubwa zaidi ni kwamba biashara hii haina msongo wa mawazo, kwani watu wengi wanahitaji bidhaa zenye kuboeresha afya, tofauti na kuuza nguo,” anasema.

Salma wa Samia anasema bidhaa za virutubisho na tiba lishe zinatumiwa na makundi mbalimbali kuanzia vijana, watu wazima na wazee.

Mwanadada Salma anasema yeye ni mfanyabiashara na mjsariamali ambaye anatamani kuibadilisha jamii ya Kitanzania ili iiachane na utegemezi ambao umaekuwa ukitawala kwa muda mrefu.

Akizungumzia uamuzi wake wa kutumia jina la Salma wa Samia Suluhu anasema yeye anamkubali sana Rais Samia na katika kuonesha upendo aliamua kujiita hivyo, ila yeye sio mtoto wa Rais Samia.

"Hainipi wakati mgumu, kujiita Salma wa Samia Suluhu, kwani nampenda na kumkubali, mimi nina dhamira njema kwani natembea katika ndoto zake," anasema.

                                     




No comments:

Post a Comment