WAPENDEKEZA ELIMU YA MILIKI UBUNIFU IFUNDISHWE KUANZIA SHULE ZA MSINGI - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Thursday, November 30, 2023

WAPENDEKEZA ELIMU YA MILIKI UBUNIFU IFUNDISHWE KUANZIA SHULE ZA MSINGI

                                               ............................................................................

NA MWANDISHI WETU

WASHIRIKI wa mafunzo ya Miliki Ubunifu katika Halmashauri ya Wilaya ya Longido wamependekeza kuwa ili idadi ya wavumbuzi Tanzania iongezeke, elimu ya Miliki Ubunifu itolewe kuanzia ngazi ya shule ya  msingi  ili kuwaandaa  wanafunzi kuwa wavumbuzi wakiwa bado wadogo.

Akichangia mada baada ya wasilisho kuhusu umuhimu wa kusajili vumbuzi mbalimbali lililotolewa na Ofisa wa  Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Benedickson Byamanyilwowa leo Novemba 30, 2023 wilayani Longido, mfanyabiashara, Elisante Mwasha amesema elimu ya Miliki Ubunifu ni muhimu kufundishwa kuanzia ngazi ya shule za msingi ili kuwajengea uelewa wa kutosha na hatimaye kuzalisha wavumbuzi wengi  nchini  na kuzisajili vumbuzi hizo BRELA .

"Elimu mliyotupatia leo ni nzuri sana lakini naona kama imechelewa na endepo ningekuwa na elimu hii muda mrefu, mbali na biashara ninazofanya ningeweza kuvumbua vitu mbalimbali na kunufaika na uvumbuzi wangu," alifafanua Mwasha.

Awali, Byamanyilwowa aliwaeleza washiriki hao kuwa pamoja na kwamba BRELA  imekuwa ikitoa elimu na kuhamasisha wadau kusajili vumbuzi zao  bado idadi  ya maombi hairidhishi.

Kutokana na hali hiyo BRELA imejikita katika kutoa elimu kuhusu Miliki Ubunifu katika vyuo vya kati na vyuo vikuu ili kukuza uelewa wa vijana kuhusu masuala ya Miliki Ubunifu  ambayo wakiizingatia itawanufaisha kwa kuwapatia ajira.

"Hakuna maisha bila hataza, vumbuzi inaongeza ajira, inamwezesha mvumbuzi kubaki katika ushindani ndani na nje ya nchi na zaidi inampa haki ya kipekee ya kumzuia mtu yoyote kutumia vumbuzi yake,"ameeleza Byamanyilwowa.

  Akielezea kuhusu  vigezo vya uvumbuzi kama ilivyoanishwa katika sheria  inayolinda uvumbuzi sura 217 amesema, uvumbuzi ni ule unaotatua changamoto katika jamii kwa kutoa suluhisho la changamoto hiyo au tatizo hilo, mfano mvumbuzi aliyevumbua miwani alilenga kutatua changamoto ya mtu mwenye tatizo la uoni hafifu wa kuona karibu au mbali, hivyo basi mvumbuzi huyo akatatua changamoto hiyo kwa kuvumbua miwani yenye lenzi za kuona karibu na kuona mbali.

Kisheria uvumbuzi lazima uwe ni mpya, uvumbuzi huo ukisajiliwa unalindwa kwa miaka 20 na mvumbuzi anachopaswa kufanya ni kuhuisha vumbuzi yake kwa kulipa shilingi 4,000/= kwa mwaka wa kwanza na baada hapo atatakiwa kuhuisha kila mwaka kwa gharama ya shilingi 1000/= , huku gharama za awali za usajili na kupata cheti nikiwa ni shilingi 22,000/=.

Kwa upande wake Ofisa Sheria wa BRELA, Andrew Malesi akiwasilisha mada kuhusu umuhimu wa kusajili logo amesema logo ni mali kama mali nyingine, hivyo endapo itasajiliwa inaweza kuuzwa au kutumiwa na mtu mwingine kwa makubaliano maalum na mmiliki wa logo husika.

Amewaeleza kuwa matumizi ya logo ni kwa wafanyabiashara wote kuanzia wadogo, wa kati na wakubwa hivyo ni muhimu wakabuni logo za biashara zao na kuzisajili ili waweze kijitofautisha sokoni, kujitangaza na hata  kutumiwa na mtu mwingine  kwa  makubaliano maalum na mmiliki wa logo husika.

BRELA iko mkoani Arusha  kuanzia Novemba 27, 2023 kutoa elimu ya Miliki Ubunifu kwa wafanyabiashara ambapo elimu hiyo imekwishatolewa kwa wafanyabiashara 182 wa Arusha Jiji,  Halmashauri ya Wilaya Arusha, Meru na Longido.






No comments:

Post a Comment