ZIARA YA RAIS DKT SAMIA ZA MOROCCO, SAUDIA ZALETA TIJA KWA WATANZANIA - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Wednesday, November 15, 2023

ZIARA YA RAIS DKT SAMIA ZA MOROCCO, SAUDIA ZALETA TIJA KWA WATANZANIA

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akizungumza kwenye Mkutano wa Waandishi wa Habari kuhusu Mafanikio ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyofanya nchini Morocco na Saudi Arabia. Mkutano huo umefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 15 Novemba, 2023.

* WAWEKEZAJI WAIGOMBANIA TANZANIA KAMA NJUGU

 *WATANZANIA WAPATA FURSA ZA AJIRA OMANI, DUBAI

NA MAGENDELA HAMISI

ZIARA ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan katika mataifa ya Marocco na Saudi Arabi imekuwa na mafanikio makubwa kutokana na kupatikana kwa fursa ya ajira kwa watanzania na wawekezaji kuhitaji kuja nchini kwa wingi.

Hayo yameanishwa na baadhi ya viongozi waliopata nafasi ya kujumuika na Rais Samia katika ziara hiyo na kutoa taarifa fupi Novemba 15mwaka huu mbele ya waandishi wa habari Ikulu jijini Dar es Salaam.

 Awali Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega, amesema kwamba Rais Samia akiwa katika mataifa hayo amefanya kazi kubwa ya kuitangaza Tanzania kuwa ina fursa ya wawekezaji kuja kuwekeza katika sekta mbalimbali za kiuchumi.

“Watanzania lazima tujue kwamba dunia ya sasa inahitaji ushirikiano katika nyanja mbalimbali za kichumi na unatakiwa kutangaza fursa ulizonazo na uwashawishi wawekezaji kwa nini waje kwako na wasiende kuwekeza katika mataifa mengine, jambo ambalo Rais wetu amefanikiwa,” amesema.

Amesema kutokana na uwezo mkubwa ambao ameonesha Rais Samia, imefanya wawekezaji kuonesha kuja kuwekeza nchini na michakato ya wawekezaji wengine inaendelea kufanikisha hayo na Saudi wamehitaji kushirikiana katika nyanja ya sekta ya usafiri wa anga, biashara ya nyama na nyinginezo ambazo zipo katika mchakato kukamilika.

Ameongeza kuwa uwepo wa ushirikiano katika sekta ya usafiri wa anga itatoa fursa kubwa wa wananchi wake kuja kwa wingi kufanya shughuli za maendeleo jambo litakalosaidia kuinua pato la taifa na mtu mmoja mmoja.

Amefafanua kuwa Tanzania imefanikiwa kuuza mbuzi na kondoo nje ya nchi kwa asilimia 80 ingawa bado haijafanikiwa kuuza ng’ombe kutokana na changamoto kadhaa na sasa wanazifanyia kazi ikiwemo eneo la chanjo na malisho.

Ulega akizungumza kuhusu uboreshaji wa nyama ili kupata soko la uhakika amesema baadhi ya wawekezaji kutoa Saudia watakuja nchini kwa lengo la kusaidiana na watanzania katika uzalishaji wa nyasi kwa ajili ya malisho ya wanyama ili kupata mifugo bora kwa mahitaji ya kibiashara.

“Hadi kufikia Julai mwaka mwaka huu Tanzania imeuza nyama nchini Saudia tani 1700 huku hitiaji ikiwa ni tani 20,000 kila mwezi na tumefanikiwa kuuza nje nyama tani 14,000 kwa kipindi hicho hivyo jitihada zinaongezeka ili kuhakikisha tunafikia mafanikio na tayari nimezungumza na wataalamu kutoka Chuo cha Kilimo (SUA) kwa ajili ya kuwekeza kwenye nyasi  bora,” amesema.

Ameongeza kuwa kinachohitajika kwa wafugaji ni kuacha ufugaji wa kimila na badala yake wafanye ufugaji wa kibiashara ili kutumia fursa hiyo vizuri na mchakato mwingine ili wa kuboresha katika eneo hilo wanapanga kila miezi mitatu kuwe na chanjo itakatofanya kuwa na mifugo bora kwa ajili ya kuuza nje ya nchi.

Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kagodosa amesema mchakato kukamilika kwa reli ya (SGR) kutoka Dar es Salam hadi Morogoro imekwamishwa na mambo kadhaa ikiwamo ucheleweshwaji kichwa ambacho kwa sasa kinafanyiwa majaribio na baadhi ya madaraja ambayo bado hayajakamilika likiwamo la Vingunguti.

Akizungumzia  kuchelewa kwa Reli ya Kusini amesema imetokana na kupitia hatua mbalimbali za kimchakato kwa nchi nne ziliingia makubaliano ya ujenzi huo miaka 19 iliyopo ambazo ni Tanzania, Msumbuji, Malawi na Zambia.

“Kihistoria ujenzi wa Reli ya Kusini inaonesha wazi haujachelewa na unakwenda vizuri kwa maana nchi husika kulikuwa na hatua mbalimbali za ujenzi wa reli na bandari upanuzi wa bandari kwa Tanzania mbayo unakwenda vizuri ,” amesema.

Naye, Mkurugenzi wa Idara ya Uhamasishaji Uwekezaji Tanzania (TIC), John Mnali amesema ziara anazofanya Rais Samia, zimefungua sekta ya uwekezaji inaashiria hadi kufikia mwaka 2025 upo uwezekano wawekezaji wakachangia shilingi trilioni 30 kwa mwaka kwa pato la taifa.                  

Amesema kutokana na Rais Samia kuzunguka dunia kutangaza fursa zilizopo Tanzania katika kipindi cha Juni  hadi Septemba 2023, TIC imesajili miradi 137 mpya ambayo itawezesha kupatikana ajira 86,900 na kwa mwaka 2022 tumesajili miradi 86 ambayo iliwezesha kupatikana ajira 12,000, ila kwa ziara za hivi karibuni ongezeko limekuwa kubwa”  amesema.     

Ameongeza kuwa licha ya ziara za Rais Samia kutangaza fursa zilizopo nchini, pia marekebisho ya sheria ya uwekezaji yamechangia ongezeko la wawekezaji hasa wazawa na kwa sasa asilimia 49 ya wawekezaji nchini ni wazawa na hilo limechangiwa na sheria nzuri iliyopo iliyoshusha mtaji wa uwekezaji kwa watanzania.

 Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mashirika ya Kati kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Abdallah Kilima amesema nchi za Mashariki ya Kati ikiwamo Dubai na Oman ambazo zinategemea zaidi nguvu kazi kutoka nje ya taifa hilo, kumekuwa na fursa nyingi za ajira ambazo watanzania wanatakiwa kuzichangamkia.

“Tumeshaingia mikataba na mashirika mbalimbali kwa ajili ya kuchukua watanzania kwenda huko kwa ajili ya kazi ikiwamo za ndani, hivyo kinachotakiwa ni wahitaji kufuata utaratibu na si kutumia njia zisizo sahihi kwa maana wanapopata tatizo tunashindwa pa kuanzia kutatua tatizo lolote litakapomkuta.

“Watanzania waondoe dhana kuwa wengi wanaofanya kazi Omani wanateseka, hilo si kweli Omani ina watanzania milioni 18 wakiwamo wafanyakazi za ndani na asilimia 92 wako salama na asilimia 8 ndio wana changamoto,  hiyo inatokana kutofuata taratibu za kuingia huko ingawa tunachukua hatua za kutatua tatizo palezinapojitokeza,” amesema .

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Masanja Kadogosa akizungumza kwenye Mkutano wa Waandishi wa Habari kuhusu Mafanikio ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyofanya nchini Morocco na Saudi Arabia. Mkutano huo umefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 15 Novemba, 2023.

Mkurugenzi wa Uhamasishaji Uwekezaji kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) John Mathew Mnali akizungumza kwenye Mkutano wa Waandishi wa Habari kuhusu Mafanikio ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyofanya nchini Morocco na Saudi Arabia. Mkutano huo umefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 15 Novemba, 2023.

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Zuhura Yunus akizungumza jambo na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega mara baada ya mkutano wa Waandishi wa habari, Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 15 Novemba, 2023.
Viongozi mbalimbali waliohudhuria Mkutano huo na Waandishi wa Habari kuhusu Mafanikio ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyofanya nchini Morocco na Saudi Arabia. Mkutano huo umefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 15 Novemba, 2023.




Waandishi kutoka Vyombo mbalimbali vya Habari nchini wakiwa kwenye Mkutano wa kuelezea Mafanikio ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyofanya nchini Morocco pamoja na Saudia Arabia . Mkutano huo na Waandishi wa Habari umefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 15 Novemba, 2023.

No comments:

Post a Comment