Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo akizungumza na waandishi wa habari katika jijini Dar es Salaam.
NA MWANDISHI WETU
MAMLAKA ya Kudhibiti
na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), imekamata Kilogramu 4.623 za aina mpya
ya dawa ya kulevya aina ya methylene dioxy pyrovalerone (MDPV) iliyokamatwa
jijini Dar es Salaam ikisafirishwa na raia wa Comoro anayeitwa Ahmed Bakar Abdou
(32).
Hayo yamebainishwa leo
Aprili 4, 2024 jijini Dar es Salaam na Kamishna Jenerali wa DCEA Aretas Lyimo
akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema Methylene dioxy pyrovalerone
(MDPV) ni dawa mpya ya kulevya iliyo katika kundi la vichangamshi inayotengenezwa
kwa kutumia kemikali bashirifu.
"Dawa hii ina
kemikali inayoweza kuleta madhara ya haraka kwa mtumiaji ikilinganishwa na dawa
nyingine za kulevya. Pia, imeongezwa nguvu ya kilevi inayozidi cocaine, heroin
na methamphetamine". Amesema.
Amesema, dawa hiyo ya
kulevya huuzwa kwa njia ya mtandao (internet) na husafirishwa kupitia kampuni
za usafirishaji vifurushi na hufichwa kwa kuwekwa chapa za majina bandia kama
vile bath salts, Ivory Wave, plant fertilizer, Vanilla Sky, na Energy.
Aidha amesema
wamefanikiwa kukamata jumla ya Kilogramu 54,506.553 za dawa za kulevya za
mashambani na viwandani pamoja na kuteketeza ekari 262 za mashamba ya bangi.
Amesema watuhumiwa 72
wamekamatwa kuhusika na dawa hizo na baadhi yao tayari wamefikishwa mahakamani.
"DCEA kwa
kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama pamoja na wakala wa misitu
(TFS) tulifanya operesheni katika mikoa ya Shinyanga, Tabora, Iringa, Mbeya,
Arusha na Dar es Salaam na kufanikiwa kukamata dawa hizi". Amesema.
Amesema dawa
zilizokamatwa ni bangi kilo 54,489.65, mirungi Kilogramu 10.3, heroin gramu
90.93, cocaine gramu 1.98 na Kilogramu 4.623 za aina mpya ya dawa ya kulevya
inayoitwa methylene dioxy pyrovalerone (MDPV) iliyokamatwa jijini Dar es Salaam
ikisafirishwa na raia wa Comoro anayeitwa Ahmed Bakar Abdou (32).





No comments:
Post a Comment