NA MWANDISHI WETU, MBEYA
KANISA la Assemblies of God la Tanzania (TAG) Jerusalem Temple lililopo Sokomatola jijini Mbeya, limetoa msaada wa magodoro 100 yenye thamani ya TZS Milioni 4.2 kwa Shule ya Sekondari Loleza ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 85 tangu kuanzishwa kwa kanisa hilo.
Akipokea msaada huo Aprili 26, 2024 kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbeya Mhe. Aziz Mohamed Fakii ameushukuru uongozi wa kanisa hilo pamoja na waumini wake kwa kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali, kuhakikisha kuwa taifa linakuwa na vijana wenye elimu ambao wataleta tija kwa Taifa la baadaye.
Mhe. Fakii amewaeleza kuwa msaada walioutoa hawajapoteza bali ni akiba hivyo ni vema kuendelea kushirikiana kwani Serikali peke yake haiwezi kuleta maendeleo bila kuungana na wananchi wake ili kuleta maendeleo ya Taifa.
"Ninawaomba muendelee kuwafikia wenye uhitaji wengine waliopo mahabusu, wagonjwa na wenye shida mbalimbali", amesisitiza Mhe. Fakii.
Awali akizungumza kabla ya kukabidhi magodoro hayo Mchungaji wa kanisa hilo Dkt. Sunday Matondo amesema kanisa hilo baada ya kufahamu kuwa kuna uhitaji wa magodoro katika shule hiyo, likaona ni vyema kutoa msaada shuleni hapo, kwani mbali ya kuhubiri kwa maneno pia wanapaswa kuhubiri kwa matendo.
Dkt. Matondo amesema maadhimisho ya miaka 85 ya Kanisa kitaifa yanatarajia kufanyika mwezi Julai, 2024, kwa sasa ni maadhimisho ya kanisa mahali pamoja, ambapo kanisa la TAG Jerusalem Temple lililopo Sokomatola linatimiza miaka 69 tangu lilipoanzishwa, hivyo kama kanisa likaguswa kutoa msaada huo unaotokana na sadaka za waumini.
Dkt. Matondo amesema Kanisa hilo limekuwa na kawaida ya kutoa misaada kwa wahitaji mbalimbali na si mara ya kwanza kutoa msaada katika shule hiyo, kwani ilishawahi kutengeneza mabeseni ya kunawia mikono.
Amesema mbali na shule hiyo ilishatoa msaada wa madawati katika shule za Msingi za Mbata na Maendeleo na msaada wa blanketi za wagonjwa na mahitaji madogo madogo kwa wauguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Wazazi Meta na vitanda vya wagonjwa na mashuka katika Kituo cha Afya cha Kiwanja Mpaka.
kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya Bi. Annamary Joseph amelishukuru kanisa hilo kwa msaada uliotoa kwani umefika wakati muafaka, hivi karibuni shule hiyo ilipata msaada wa vitanda ambavyo vilikuwa vinahitaji kuwekwa magodoro.
Naye Mkuu wa Shule hiyo Bi Tumtukuze Mpindo na Mwakilishi wa wanafunzi, Bi. Jackline Mirocho wameshukuru kwa roho Mtakatifu kuliongoza kanisa hilo na kuamua kwenda Loleza kuwapatia msaada na kuahidi kuyatunza na kutowaangusha kitaaluma na kimaadili.h
No comments:
Post a Comment