NA MWANDISHI WETU, MBEYA
SERIKALI imepanga kutoa viwanja 21 kwa waathirika wa maporomoko ya tope katika Mlima Kawetere, Itezi jijini Mbeya, huku zaidi ya vifaa na vyakula vyenye thamani ya Shilingi Milioni 40 vikitolewa kuanziaAprili, 14, 2024 maafa hayo yalipotokea hadi sasa.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa kwa ajili ya waathirika, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini ambaye pia ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani(IPU), Dkt. Tulia Ackson ametoa pole kwa wahusika na kumshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa misaada ya chakula, magodoro, fedha taslimu na viwanja.
Aidha Dkt. Tulia amewaomba wadau wengine watakaoguswa na jambo hili kuchangia vifaa vya ujenzi ili kufanikisha kupatikana kwa sehemu ya kujihifadhi waathirika hao, baada ya nyumba zao kufukiwa na tope.
Kwa upande wake, William Lukuvi akiwakilisha ujumbe kutoka Ofisi ya Rais amesema kuwa Mhe. Rais ameguswa na kila eneo lililokumbwa na maafa hapa nchini na bado ataendelea kutoa msaada kwa waathirika
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amekiri kupokea maelekezo kutoka kwa Mhe. Rais na kuahidi kutoa viwanja sehemu nzuri na utekelezaji utaanza mara moja.
Mhe. Dkt. Tulia amefika Itezi leo tarehe 21 Aprili, 2024 na kuzungumza na wahanga pamoja na kutembelea eneo ulipotokea mmomonyoko wa tope katika mlima Kawetere.
No comments:
Post a Comment