NA BEATUS MAGANJA
MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA leo Aprili 24, 2024 imepokea meli ya watalii wapatao 230 kutoka Mataifa mbalimbali Duniani waliofika katika Hifadhi ya Urithi wa utamaduni wa Dunia ya Magofu ya Kilwa kisiwani na Songo Mnara kwa ajili ya shughuli za utalii.
Meli ijulikanayo kwa jina la "Silver Clouds" ndiyo iliyotia nanga katika Hifadhi hiyo ikiwa imebeba watalii kutoka Mataifa ya Australia, Ubeligiji, Brazil, Canada, Chile, China, Ujerumani, Ireland na Norway huku watalii wengine wakitokea Mataifa ya Italia, Ureno, Africa ya Kusini, Hispania, Sweden, Switzerland, Ukraine, Uingereza na Marekani.
Huu ni mwendelezo wa safari za watalii kutoka kona mbalimbali za Dunia kuja kujionea fahari ya urithi wa Dunia wa utamaduni, historia na malikale uliopo katika Hifadhi hiyo inayosimamiwa na TAWA.
Ikumbukwe kuwa Hifadhi hii imekuwa ikipata wageni wengi wa ndani na nje ya nchi yetu ambapo hivi karibuni (Februari, 2024) Hifadhi hiyo ilipokea zaidi ya watalii wa nje 900 kutoka sehemu mbalimbali Duniani kwa ajili ya shughuli za utalii, idadi inayotajwa kuvunja
rekodi katika Hifadhi hiyo.
Watalii hao wakiongozwa na Kampuni ya Utalii ya Takim Holidays walipokelewa na kukaribishwa kwa ngoma za asili ya watu wa Kilwa Kisiwani iitwayo kitupolo ambayo iliwafanya waonekane kuwa na bashasha muda wote
Tanzania inaendelea kunufaika na kazi kubwa iliyofanywa na Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipocheza filamu maarufu ya Tanzania The Royal Tour ambayo imefungua milango kwa watalii wengi kuingia nchini kwa ajili ya shughuli za utalii.
No comments:
Post a Comment