NA WAF- DAR ES SALAAM
UTARATIBU mpya wa kitaifa wa upimaji wa Virusi vya UKIMWI kwa vipimo vitatu ili kuthibisha kuwa mtu ana maambukizi ya VVU utasaidia kuongeza wigo wa upimaji wa VVU nchini.
Hayo ameyasema Kaimu Meneja Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI, magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini Dkt. Ona Machangu l Julai 02, 2024 Jijini Dar es Salaam katika ufunguzi wa kikao cha kutambulisha mwongozo mpya (Algorithim) ya kitaifa kuhusu upimaji wa Virusi vya UKIMWI, ambapo mtu atapimwa ama kujipima na kugundulika kuwa na virusi vya UKIMWI kwa kipimo cha awali atalazimika kupima vipimo vingine viwili vya uhakiki ili kuthibisha kuwa anamaambukizi ya VVU.
Dkt. Machangu amesema lengo mahususi la kutumia vipimo vitatu ni kuhakikisha wigo wa upimaji unaongezeka kwa kupima vipimo ambavyo vitaleta majibu sahihi zaidi ili kuleta manufaa na kusaidia huduma za uchunguzi kwa watu ili waweze kushawishika kupima na kuanza dozi mara moja endapo watagundulika.
Pia Dkt. Machangu amesema ili kufikia lengo la kutokomeza maambukizi mapya ya UKIMWI mwaka 2030, Wizara ya Afya inalenga kuendelea kuboresha huduma za upimaji lli kuhakikisha kila mtu anafikiwa na huduma za upimaji na kujua hali yake ya kiafya.
"Tanzania tupo katika malengo ya kidunia ya 95 95 95 na kutokana na tafiti za viashiria zinaonesha 95 ya kwanza ya upimaji kama nchi tupo asilimia 83 hivyo tunalengo hasa la kuhakikisha tunamfikia kila mtu na huduma za upimaji nchini"
Aidha Dkt. Machangu amewasihi wananchi kuendelea kujitokeza kupima afya zao ili kutambua hali zao za kiafya na kuanza dozi ya kupunguza makali ya VVU mara moja
"Niwakaribishe watanzania kufika kwenye vituo vya afya kupata huduma za upimaji pia kuna huduma za kujipima kwani ni vizuri kujua afya yako ili kufurahia maisha". Amesema Dkt. Machangu.
Kwa upande wake Mwakilishi kutoka shirika la Afya Duniani (WHO), Maria Kelly amesema kama wadau wa maendeleo wamejidhatiti kwa kuendelea kusaidiana na Serikali ili kuhakikisha mpango huo wa upimaji unaweza kutekelezeka.
No comments:
Post a Comment