RITA YATOA VYETI 195,000 - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Sunday, August 18, 2024

RITA YATOA VYETI 195,000

Kabidhi Wasii Mkuu na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini nchini (RITA), Frank Kanyusi   akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari (awapo pichani)  jijini Dar es Salaam juu  changamoto zilizojitokeza  kwenye uhakiki wa vyeti vya kuzaliwa na vifo.

NA MWANDISHI WETU

WAKALA wa Usajili , Ufilisi na Udhamini  (RITA) imesema kuwa katika kipindi cha miezi miwili iliyopita imepokea jumla ya maombi 198,972 ya vyeti vya vizazi na vifo na kati  ya maombi hayo  jumla ya waombaji 195,771  ambayo ni sawa na asilimia 98.4 tayari wamepatiwa vyeti vyao.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana,  Ofisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Frank Kanyusi amesema kuwa kati ya maombi hayo, maombi 179,485 yalikuwa ni ya uhakiki wa vyeti vya kuzaliwa  na maombi mengine 19,487 ni ya uhakiki wa vyeti vya vifo.


“Maombi mengine 18,341 yalikuwa  ya mapungufu ya vyeti hivyo ambapo wahusika walirudishiwa kwa ajili ya kufanya marekebisho,” amesema Kanyusi na kuongeza kuwa maombi 562 yalikataliwa kwa sababu vyeti vilivyowasilishwa kwa uhakiki havikuwa halali.


Kwa mujibu wa Kanyusi maombi mengine 3,201 yanaendelea kufanyiwa kazi na yatakamilika ndani ya siku chache zijazo.


Amesema  kumekuwa na changamoto kadhaa ambazo zilichangia zoezi hilo kulegalega kutokana na changamoto ya kimtandao iliyojitokeza, ambapo kikundi kazi cha taasisi hiyo kilichukua hatua za haraka kutatua changamoto hiyo.


“Licha ya changamoto hiyo ya kimtandao  kumekuwa na changamoto tofauti tofauti kutoka kwa waombaji ambazo zimefanya baadhi ya waombaji kutokubaliwa kuhakiki vyeti vyao ikiwemo kuambatanishwa kwa nakala zisizosomeka ambazo maandishi yake yamefifia, hivyo kuwafanya wataalumu kushindwa kusoma,” amesema.


Kanyusi amesema kuambatanisha nyaraka isiyo sahihi, mfano cheti cha kuzaliwa badala ya cheti cha kizazi  imefanya baadhi ya vyeti kushindwa kuhakikiwa na pia kumekuwa na makosa ya baadhi ya nyaraka kuwekwa nywila (password), hivo wakala kushindwa kuzihakiki.


Akifafanua zaidi, Ofisa Mtendaji Mkuu huyo amesema kumekuwa na makosa ya kutuma nakala ya vyeti vilivyotolewa nje ya nchi ambavyo RITA haina mamlaka ya kuvihakiki sambamba na wengine kushindwa kufuatilia majibu yao ya uhakiki katika akaunti  walizofungua hivyo kuchangia ongezeko la malalamiko.


“Changamoto tulizokutana nazo zilikuwa ni nyingi lakini kwa kushirikiana na wataalamu wetu tuliendelea kuzitafutia ufumbuzi wa haraka. Kwamfano wapo baadhi ya waombaji wamekuwa wakichagua sababu ya kuomba uhakiki tofauti na inayotakiwa ya kuomba mkopo wa elimu ya juu,”amesema.


Kanyusi amesema RITA  imeendelea kutoa elimu kwa baadhi yao wanaofika katika ofisi zake pamoja  na kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii.


Mbali ya vyeti vya uzazi na vifo, amesema  RITA pia hupokea mombi ya wanafunzi wanaoomba vyeti vya kuzaliwa kwa ajili ya kukidhi moja ya vigezo  vilivyowekwa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ya kupata mkopo.


Kanyusi amewataka waombaji wa mikopo ya elimu ya juu kutumia vyema muda uliobaki  kuhakiki vyeti vyao vya  kuzaliwa na vifo ndani ya wakati ili waweze kuwa na sifa ya kupata mikopo hiyo.


Amesema zoezi la kupokea vyeti hivyo litafungwa siku chache zijazo na hivyo kuwataka wanafunzi hao kutuma maombi yao kupitia mitandao yao kijamii ya RITA ili waweze kujua vigezo vya kukidhi maombi yao.

No comments:

Post a Comment