TNBC YAWATAKA WATANZANIA KUJIANDAA NA UCHUMI WA KIDIJITALI - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Sunday, August 18, 2024

TNBC YAWATAKA WATANZANIA KUJIANDAA NA UCHUMI WA KIDIJITALI


NA MWANDISHI WETU

SERIKALI imewataka watanzania kuwa tayari kwa utekelezaji wa mpango wa uchumi wa kidijitali ili Tanzania iende sambamba na mahitaji  ya dunia katika kuchochea mabadiliko ya uchumi.


Akizungumza wakati wa kikao cha tatu cha Kikundi Kazi Cha TEHAMA cha Baraza la Taifa la Biashara ( TNBC), Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia Mohamed Abdulla amesemaTanzania lazima ishiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali katika kipindi cha miaka 10 ijayo.


 Abdulla ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kikundi Kazi hicho,amesema mapinduzi ya uchumi wa kidijitali yatatoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi kupitia biashara, upatikanaji wa huduma na manunuzi.



“Lengo ni kuifanya Tanzania kuwa na uchumi mkubwa wa kidijitali ili iwe na ushindani katika soko la Dunia,” amesema na kuongeza kuwa utekelezaji wa mpango huo utachagiza ukuaji wa sekta nyingine mbalimbali ikiwemo kilimo, biashara na utalii.


Abdulla amesema dunia sasa imebadilika na matumizi ya mtandao katika kufanya biashara yamerahisisha upatikanaji wa huduma na kuchangia uchumi kwa kasi kubwa na hivyo Tanzania haina budi Kwenda sambamba na kasi hiyo.


“Tayari hivi sasa tunaona maendeleo  katika baadhi ya upatikanaji wa huduma, unaweza kununua huduma au bidhaa ukiwa nyumbani kwa njia ya kidijitali na huku ndiko tunataka tufike katika huduma zingine ili kurahisisha maendeleo.” Amesema.


Amesema matumizi ya uchumi wa kidijitali ndiyo mwelekeo wa dunia kwa sasa na Tanzania kama nchi imedhamiria kuhakikisha kuwa ndani ya kipindi cha miaka 10 kila kitu kiwe kidijitali.


“Kikao kilikuwa na kazi ya kujadili hatua za utekelezaji wa mpango huo wa uchumi wa kijiditali kupitia ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi,” alisema na kuongeza kuwa pamoja na mambo mengine, wajumbe wa mkutano huo walijadili mapendekezo na utekelezaji na namna ya kufanya ufuatiliaji na tathmini ili wadau wayapitie.


“ Rais Dkt Samia Suluhu Hassan tayari alishauzindua mkakati  huu, hivyo nawaomba wananchi wa mijini na vijijini wajiandae kwa utekelezaji wake,”, amesema Bw Abdalla.


Naye Mwenyekiti  Mwenza  wa kikundi kazi hicho, Jackline Uiso amesema kikubwa zaidi wanaangalia namna sekta ya mawasiliano inavyoweza kusaidia ukuaji wa uchumi wa sekta mbalimbali kupitia mapinduzi ya kidijitali, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kufanikisha mpango huu.


Amesema kuwa mkakati huo wa miaka 10 una miongozo mbalimbali kwa kila sekta katika kuhakikisha inajiandaa vipi na mapinduzi haya ya uchumi wa kidijitali.


Amesema kwa upande wa Tanzania, sekta ya fedha inaonekana kufanya vizuri kupitia miamala mbalimbali inayofanyika, lakini mikakati ni kuona sekta nyingine kama vile kilimo, afya, habari, ujenzi na elimu nazo zinajikita zaidi katika uchumi huo na kuchangamkia fursa zilizopo.


“Nchi nyingi duniani sasa hivi zinaweka nguvu katika uchumi wa kidijitali na mapinduzi makubwa yanafanyika kupitia teknolojia katika kurahisisha utoaji na upatikanaji wa huduma,”aslisema Bi Oiso.



kwa upande wake,  Katibu Mtendaji wa TNBC, Dkt Godwill Wanga amesema kuwa  mkutano huo umehusisha wadau mbalimbali ambapo mapendekezo yake tayari yamepitishwa na kikao hicho.


Amesema kuwa wataalamu watatembelea kila sekta ili kuhakikisha   mpango  huo unajulikana, kutoa elimu na kuhamasisha utekelezaji wake na hivyo kuwataka wananchi kuunga mkono mpango huu na kuwa tayari na mageuzi haya ya kidunia ambayo hayaepukiki .


Naye mjumbe wa kikosi hicho, Dkt  Nkundwe Moses Mwasaga, ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama amesema kuwa mpango huo mkakati utaangalia kipi cha kufanya ili kufikia malengo hayo.


“Moja ya mipango ni pamoja na kutoa elimu kwa wananchi na kuhakikisha malipo ya huduma mbalimbali yanafanyika kwa njia ya mtandao ili kufikia malengo,” alisema na kuongeza kuwa ni

vizuri kuhakikisha sekta zote za kiuchumi ziwe kidijitali, mifumo iweze kufanya kazi pamoja na kila Mtanzania awe na namba ya kidijitali itakayosaidia katika upatikanaji wa huduma.


Naye Profesa Wangwe, ambaye ni mjumbe wa kikosi kazi amesema kuwa maeneo ya kuweka mkakati ni mengi ili  kuangalia mchango wake katika ukuaji wa uchumi, ajira na kuiwezesha mifumo kufanya kazi pamoja ili kurahisisha manunuzi ya biashara na upatikanaji wa huduma na bidhaa. 


No comments:

Post a Comment