TAKUKURU KINONDONI YABAINI MAPUNGUFU KATIKA MIRADI SITA YENYE THAMANI BIL. 8/= - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Monday, August 5, 2024

TAKUKURU KINONDONI YABAINI MAPUNGUFU KATIKA MIRADI SITA YENYE THAMANI BIL. 8/=


NA HALIMA MWAMBA

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkoa wa Kinondoni imebaini mapungufu katika miradi sita yenye thamani ya Shilingi bil. 8, 056, 860, 672 katika kipindi cha miezi mitatu ya ufuatiliaji wake na wahusika wameshauriwa kuyarekebisha.

Akizungumza leo, Agosti 5, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa mbele ya waandishi wa Habari ya utendaji kazi wa ofisi hiyo kwa kipindi cha miezi mitatu, Elizabeth Mokiwa ambaye ni Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kinondoni amesema kutokana na mapungufu hayo wamejipanga kufuatilia ili kuhakikisha inarekdebishwa na inakamilika kwa wakati na ubora stahiki.

“Kutokana na mapungufu yalijitokeza Takukuru Mkoa wa Kinondoni tulitoa ushauri ambao umefanyiwa kazi kwa asilimia kubwa ikiwemo kuweka njia za watembea kwa miguu katika mradi wa barabara ya Nyota Njema  Kunduchi ambao utekelezaji wake ulitengewa bajeti  y ash. Bil 1,830,401,197.04 na imeanza kutekelezwa,” amesema.

Ameongeza kuwa mradi mwingine ambao ulifuatiliwa na umekamilika ni Uboreshaji Huduma ya Maji Safi (Dawasa), uliopo Wazo wenye thamani ya Sh. Bil. 3,434,722,421,03. Pia mradi wa Vikundi vya Usafi wa Mazingira katika Manispaa ya Kinondoni wenye thamani ya sh. Mil 322,586,075 fedha zilizotokana na mkopo  kutoka Halmashauri, ufuatiliaji wake ulibaini ucheleshwaji wa baadhi ya marejesho .

Kutokana na changamoto hiyo, Mokiwa ameweka wazi kuwa mchakato wa ufuataliaji unaendelea ili kuhakikisha fedha zilizokopwa zinarejeshwa kwa wakati kulingana na makubaliano ya mkataba na zoezi la usafi wa mazingira linafanyika kwa ufanisi.

Mokiwa ameongeza kuwa mradi mwingine ambao umefuatiliwa ni wa ujenzi wa boksi Kalavati katika eneo la Stop Over kwa Kapinga, wilayani Ubungo wenye thamani ya sh. mil 258, 589,000 ambapo katika kipindi hicho ulikuwa haujakamilika kutokana na kuwepo kwa changamoto kadhaa.

Amefafanua kuwa moja ya changamoto ni mkandarasi kutoweka ‘Stone Pitching’ na kusababisha kingo za daraja kubomoka,pia baadhi ya mifereji ilikuwa haijakamilika na barabara ya eneo la daraja haikuwekwa kifusi na hakuwa ametoa udongo pembezoni mwa mto uliokuwa umechimbwa wakati wa ujenzi.

Amesema mradi huo ulitakiwa kukamilika Jan 8, mwaka huu na haukukamilika kutokana na changamoto ya mvua hivyo mkandarasi akaongezewa muda hadi Mei 22, 2024 na baada ya kukaguliwa kwa mara ya pili ukawa umekamilika kwa wakati.

Mradi mwingine ambao ulikuwa umefuatiliwa ni Ujenzi wa Kituo cha Afya Kinondoni wenye thamani ya sh. bil 1, 641, 561, 979.60 na baada ya ufuatiliaji wake na kutolewa mapendekezo na kufanyiwa kazi ukakamilika na kuanza kufanya kazi.

 Mokiwa ameongeza kuwa mradi wa sita ni Ufungaji Pampu ya Maji Kibamba , Kisarawe wenye thamani ya sh. Mil 569, 000,000 ambao wakati wa ufuatiliaji wake ulikuwa umekamilika ingawa changamoto iliyojitokeza ilikuwa ni pampu kuvuja na kuathiri ubora wa mradi.

Kulingana na changamoto hiyo Mkurugenzi wa Dawasa, aliandika barua na kutoa mapendekezo ya kutatua kero hiyo na ukaguzi ulipofanyika kwa mara ya pili, tatizo hilo likawa limetatuliwa na kukamilika vema.

 



 

No comments:

Post a Comment