Kamishna Jenerali wa DCEA ,Aretas Lyimo akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Nov. 25, 2024
NA MWANDISHI WETU
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za
Kulevya(DCEA) imeelezwa kuwa baadhi ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya
wamekuwa wakipangisha nyumba na kisha kugeuza kama maghala ya kuficha dawa hizo
,hivyo imewataka wamiliki wa nyumba kuwa makini na watu wanaowapangisha.
Akizingumza leo jijini Dar es Salaam, Kamishna
Jenerali wa Mamlaka hiyo Aretas Lyimo alipokuwa akitoa taarifa ya kukamata dawa
za kulevya zaidi ya kilo 2,207 katika Mkoa wa Dar es Salaam na Tanga amesema
kuna wafanyabiashara wa dawa hizo wanapangisha nyumba lakini hawaishi zaidi ya
kuhifadhi dawa za kulevya.
"Mamlaka inatoa rai kwa wamiliki wa nyumba
kuwa makini wanapopangisha nyuma zao kwani nyumba inayotumika kwa shughuli za
dawa za kulevya ni kinyume cha sheria na inaweza kutaifishwa.
"Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za
Kulevya sura ya 95 imeweka katazo kwa mmiliki au msimamizi wa nyumba,msimamzi
wa eneo au chombo cha usafirishaji kuruhusu vitumike kwa lengo la kutengeneza
,kuvuta,kujidunga ,kuuza au kununua dawa za kulevya,"amesema Kamishina
Jenerali Lyimo.
Aidha amesema mmiliki anapojua kuwa kosa
linatendeka kwenye eneo lake analojukumu la kutoa taarifa kwa Mamlaka.Kushindwa
kufanya hivyo ni kosa la jinai na akitiwa hatiani adhabu yake inaweza kuwa
faini kuanzia Sh.mil 5 hadi Sh.milioni 50 au kifungo cha miaka mitano
hadi 30 jela au vyote kwa pamoja.
Amesema kuwa hata katika operesheni ambayo
wanaendelea kuifanya ya kusaka wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya
Kuna watuhumiwa wamepanga nyumba Kigamboni lakini wenyewe wanaishi Mabibo na
hivyo nyumba waliyopangisha inatumika kuficha tu dawa.
Amefafanua kuwa wafanyabiashara wa dawa za kulevya
ambao wanapangisha nyumba hizo wamekuwa na usiri kiasi hata mlinzi anaweza kuwa
analinda nyumba lakini haijui inatumiwa kuficha dawa za kulevya.
Hata hivyo amesema Mamlaka inatoa shukrani kwa
wananchi wanaotoa ushirikiano kwa kuwafichua watu wanaojihusisha na dawa za
kulevya na wanahimiza wananchi kuendelea kutoa taarifa.





No comments:
Post a Comment