WASANII WA FILAMU WAPONGEZWA KWA KUBEBA MAONO YA RAIS DKT. SAMIA KUTANGAZA UTALII - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Sunday, November 3, 2024

WASANII WA FILAMU WAPONGEZWA KWA KUBEBA MAONO YA RAIS DKT. SAMIA KUTANGAZA UTALII


NA JOYCE NDUNGURU

UMOJA wa Waigizaji Mkoa wa Dar es Salaam wapongezwa kwa kubeba maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutangaza utalii.  


Maneno haya yamesemwa Novemba 2, 2024 na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule katika tamasha la "Shtuka, boresha afya ya akili ndani ya Hifadhi ya Pande" lililoandaliwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa kushirikiana na Umoja wa Waigizaji Mkoa wa Dar es Salam.


"Niwapongeze wasanii wa sekta ya uigizaji kwa kubeba maono ya Rais Samia ya kuitangaza sekta ya utalii na hasa, Hifadhi yetu ya Pande ambayo inapatikana kwenye Wilaya yetu ya Kinondoni", amesema Mhe. Mtambule.


"Pia tuendelee kutumia akaunti zetu za mitandao ya kijamii kuhamasisha makundi mbalimbali ili yaweze kuja kutembelea hifadhi ya Pande" aliongeza Mhe. Mtambule.


Pia Mtambule, aliwashukuru wasanii kwa kutembelea hifadhi hiyo na alisisitiza kuwa utangazaji wa shughuli za utalii ukiongezeka wageni watafurika na hivyo uchumi wa Nchi utakua.


Kadhalika, Mtambule ameipongeza TAWA kwa jitihada zake katika kuboresha hifadhi ya Pande kwa kuongeza mazao mbalimbali ya utalii ikiwemo uanzishwaji wa bustani ya wanyamapori mbalimbali wakiwemo Simba, Duma, Chatu, Mamba, Nyumbu, Pundamilia nk


Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, William Kitebi akimuwakilisha Kamishna wa Uhifadhi TAWA, alitoa shukrani zake za dhati kwa Mtambule kwa ushirikiano wake na TAWA katika masuala ya uhifadhi wa hifadhi za Pande na Kunduchi. Vilevile aliwashukuru Umoja wa waigizaji Mkoa wa Dar es Salaam kwa kuja kutembelea hifadhi ya Pande.


Naye, Mwenyekiti wa Umoja wa waigizaji Mkoa wa Dar es Salaam, Leonard Mwinuka amesema wao kama wasanii wataendelea kumuunga mkono Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika utangazaji wa utalii. Pia aliishukuru uongozi wa TAWA kupitia Hifadhi ya Pande kwa kuwapa ushirikiano wa kutosha, " Mbegu mliyopanda kwetu, itaota na tutakuwa mabalozi wazuri wa kuelezea uzuri wa hifadhi hii" alisisitiza Mwinuka.

Tamasha hilo lilihudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa TAWA pamoja na Bodi ya Utalii Tanzania ( TTB) wakiwemo Kamishna Msaidizi Mwandamizi anayeshughulikia huduma za biashara, Hamza Hassani, Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Sylvester Mushy.

Wengine ni Mkurugenzi wa Masoko kutoka TTB, Ernest Mwamaja pamoja na Kamanda wa Pori la Akiba Pande, Dorothea Massawe.

Aidha, tamasha hili liliambatana na zoezi la uchangiaji wa damu salama.

 





No comments:

Post a Comment