NA MWANDISHI WETU
UJENZI wa Jengo la kutolea huduma ya mama na Mtoto uliofanywa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii(TASAF) katika kituo cha afya cha Makole Jijini Dodoma umesaidia kuwezesha wananchi kupata huduma katika mazingira bora na rahisi.
Kabla ya Ujenzi wa jengo hilo wananchi wa Kata ya Makole hasa waliokuwa wakifuata huduma za Mama na Mtoto zikiwemo za chanjo walikuwa wanapatiwa huduma katika turabai lililokuwa limefungwa katika kituo hicho na kusababisha utolewaji huduma kutakuwa mazingira rafiki.
Akizungumza kuhusu ujenzi wa jengo hilo uliofanywa na TASAF , Mtendaji wa Kata ya Makole Suzan Yohana amesema kabla ya jengo kujengwa wananchi walikuwa wanapata adha kubwa ikiwemo ya kunyeshewa mvua wakati wa msimu wa mvua,vumbi lakini na kukosa hewa safi kwasababu ya ufinyu wa eneo ambalo lilifungwa turubai.
“Kata ya Makole ni kubwa sana hivyo watu walikuwa wanatoka maeneo mbalimbali kuja kupata huduma ya kliniki ya mama na mtoto .Mazingira eneo la utoaji huduma halikuwa rafiki kwani lile turubai halikuwa nzuri na lilikuwa halifai kwa matumizi.Kwa sasa tunashukuru tumepata jengo nzuri na wananchi wanapata huduma katika mazingira mazuri,”amesema.
Ameongeza kuwa wanaishukuru TASAF kwani wamapeleka faraja katika huduma za mama na mtoto na kwa sasa wananchi wamekuwa wakipata huduma katika mazingira mazuri,safi na salama.
“Imekuwa faida kwetu na tunawashukuru TASAF kwa kujenga jengo hili ambalo sasa limesaidia huduma kutolewa katika mazingira bora zaidi.TASAF wamekuwa wadau wazuri sana katika kuboresha huduma hizi za mama na mtoto,”amesema Yohana.
Kwa upande wake Joyce Kimario ambaye ni Kaimu Muuguzi Mfawidhi wa Kituo cha Afya Makole Mkoani Dodoma amesema kabla ya jengo hilo la TASAF walikuwa wakitoa huduma katika mazingira magumu.
“Siku za nyuma tulikuwa tunatoa huduma ya chanjo ya mama na mtoto chini ya miaka mitano katika turubai lakini baada ya TASAF kuona mazingira yalivyokuwa mwaka jana wakatujengea jengo nzuri ambalo tunalitumia.”
Wakati huo huo Muuguzi Mkunga katika kituo hicho Tumain Myeule amesema wa wanashukuru kwani wananchi wanafurahia huduma baada ya kujengwa jengo hilo na wameomba TASAF.”Tunawashukuru TASAF kwa ujenzi wa jengo hilo.”
Awali Mwanakamati anayeshughulikia mpango wa walengwa wa TASAF ngazi ya mtaa Neema Tandi amesema wananchi wa Kata ya Makole ambao ndio walengwa kwa jengo hilo wanafurahia huduma kwani huko nyuma walikuwa wakizipata katika mazingira magumu.
“Wakati kukiwa na turubai kuna muda huduma zilikuwa zinasimama kwa mfano upepo au mvua zilikuwa zinasababisha turubai linaanguka hivyo huduma zinasimama,Leo hii tumepata jengo hili ambalo limejengwa na TASAF mwaka jana,walengwa wanafurahia huduma za chanjo ya mama na mtoto.”
Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa Kata ya Makole wametoa pongezi kwa TASAF kwa kuona umuhimu wa kujenga jengo hilo ambalo limewezesha kuwa wanapata huduma katika mazingira mazuri ukilinganisha na ili ilivyokuwa kabla ya kujengwa kwa jengo hilo.
No comments:
Post a Comment