NA MWANDISHI WETU
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila leo Januari 22, 2025 ameongoza kikao cha Baraza la Biashara mkoani humo.
RC Chalamila wakati anafungua kikao hicho amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara hapa nchini hususani Mkoa wa Dar es Salaam
" Rais ameunda timu ya watalaam wabobevu kupitia masuala ya kikodi kwa lengo la kuja na suluhu ya malalamiko ya wafanyabiashara kuhusu kodi kandamizi hii ni ishara yake dhamira njema, " amesema.
Kupitia kikao hicho alitoa nafasi kwa wafanyabiashara kueleza changamoto na vikwazo vya kibiashara, ushauri, maoni pamoja na mapendekezo yao vilevile ufafanuzi wa maeneo ambayo yalikuwa yakilalamikiwa siku za nyuma kama yamefanyiwa kazi au la!
Aidha RC Chalamila amewahakikishia wafanyabiashara kuwa Mkoa utaendelea kuweka mipango ya maendeleo ya kibiashara kupitia maoni na ushauri unaotolewa katika vikao vya mabaraza ya Biashara Mkoa pia amewataka kutumia vizuri fursa zilizoko ikiwemo kufanya biashara saa 24 pamoja na fursa za Uchumi wa bluu.
Kwa upande wa Katibu Tawala wa Mkoa Dkt Toba Nguvila amesema kikao hicho ni muhimu kwa masilahi mapana ya maendeleo ya Biashara katika kukuza uchumi wa Mkoa na Taifa hivyo ameahidi kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa pia kuhakikisha vikao hivyo vinafanyika kama inavyoelekezwa kwa mujibu wa sheria katika ngazi ya Mkoa na wilaya zote tano.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la wafanyabiashara Mkoa, Denis Chacha ametoa rai kwa wafanyabiashara wa Mkoa huo kutoa ushirikiano kwa Serikali ili kuzipatia ufumbuzi changamoto zao ambapo amesema watafanya kikao chao ili kutoa fursa zaidi za kueleza changamoto zao
Mwisho kikao hicho kimehudhuriwa na wafanyabiashara, wawekezaji, watalaam wa kutoka Wizara ya biashara, Sekretariati ya Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri na makatibu Tawala wa Wilaya zote za Mkoa.
No comments:
Post a Comment