NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR
MAMLAKA ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) na wadau wake jana Januari 7, 2025 wamekabidhi hundi ya mfano ya shilingi milioni 321 kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla ikiwa ni mwitikio wa Sekta ya Bima nchini kuunga mkono Maadhimisho ya 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Kilele cha Maadhimisho ya 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar kitafanyika tarehe 12 Januari 2025 Uwanja wa Gombani, Pemba.
Hundi hiyo imekabidhiwa na Naibu Kamishna wa Bima Tanzania, Khadija Said ambapo ameeleza kuwa hatua hii ni utekelezaji wa ahadi ya sekta ya bima nchini ya kuwa sehemu ya maadhimisho hayo ili kuibua na kuchochea ushirikiano wenye tija na Serikali hususani kwenye miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa hapa nchini kuona namna kampuni za bima za nchini zinavyoweza kushiriki kwenye kukinga majanga.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Umoja wa Kampuni za Bima Tanzania (ATI) Wilson Mnzava ambae pia ni Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Bima ya CRDB (CIC) ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), kwa kushirikisha Kampuni za Bima katika tukio hilo muhimu.
Amesema” huu ni mwanzo na wanaahidi kutaendelea kushiriki kila mwaka ili kuhakikisha kwamba sekta ya bima nchini inakua ni miongoni mwa mafanikio ya maadhimisho haya”
Aidha, Wilson ameiomba SMZ kutoa fursa kwa kampuni za bima za nchini ili ziweze kushiriki kwenye kukinga miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa chini ya serikali na wawekezaji binafsi.
Akipokea hundi hiyo Makamu wa Pili wa Rais Abdulla ametoa shukrani za dhati kwa sekta ya bima nchini kwa hatua hii akisema mchango huu ni mkubwa na wanauthamini.
"Fedha hizi mlizochanga zitatumika kama ilivyokusudiwa. Tuendelee kufanya kazi kwa juhudi tukiwa na matarajio kuwa kazi inayofanyika kwenye sekta ya bima nchini ni kwa ajili ya Watanzania na kuleta ushirikiano wenye tija, natoa wito kwa kampuni za bima nchini kuchangamkia fursa za biashara zilizopo na ofisi yangu ipo tayari kutoa msaada pale inapohitajika,” amesema.
No comments:
Post a Comment