NA MWANDISHI WETU
MWENYEKITI wa Chama Cha Wananchi (CUF) Taifa, Profesa Ibrahimu Lipumba amesema ujenzi wa demokrasia nchini ambao amedai unaporomoka ni hukumu la Watanzania wote bila kujali itikadi.
Prof. Lipumba amebainisha hayo leo, Januari 8, 2025 jijini Dar es Salaam, wakati akifungua kikao cha Baraza Kuu cha Chama hicho cha kwanza tangu kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa chama hicho.
Ameongeza kuwa demokrasia hiyo ambayo inaonekana kuporomoka si kwa Tanzania pekee bali duniani kote na hiyo ni kwa majibu ya tafiti ambayo imefanywa na wataalamu.
Amesema kwamba kutokana na changamoto hiyo kuanza kuonekana hapa nchini, amemsihi, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kusimamia ipasavyo falsafa yake ya 4R ili kuendelea kuimarisha Demokrasia nchini.
Aidha amesema kwamba kwa upande wa Tanzania kuporomoka kwa Demokrasia imejidhihirisha katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliyofanyika Mwaka 2024 hivyo amesema Rais Dkt Samia Suluhu Hassan anajukumu la kuhakikisha dosari zilizojitokeza katika uchaguzi huo wa 2024 na 2020 hazijitokezi tena.
" Hali ya Demokrasia Duniani ilikua ikiporomoka ,wataalamu wa mambo ya Demokrasia wanaonesha katika tafiti tangu Mwaka 2006 ,Demokrasia imekua ikiporomoka Duniani.
" Hata Marekani ambalo pamoja na mapungufu mengi ndiko utaratibu wa Demokrasia ulipoanza kwa kuweza kuchagua viongozi wa kuwawakilisha wananchi nako Demokrasia imekua ikiporomoka." amesema Prof.Lipumba
Aidha ameongeza kuwa hata uchaguzi uliopita wa Marekani wa kumchagua Rais Donald Trump ambaye Mwaka 2020 aliyakataa matokeo ya uchaguzi inaonesha namna Demokrasia ilivyoporomoka nchini humo.
No comments:
Post a Comment