NA MWANDISHI WETU
MRADI wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) umeshinda tuzo ya kujali Afya na Usalama kazini kwa mwaka wa 2024/2025 inayotolewa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Afya na Usalama Kazini (TOHASA) katika hafla iliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
Lengo la tuzo hiyo zilizoandaliwa ni kuhamasisha usalama na afya katika maeneo ya kazi na kuepusha madhara yanayoweza kutokea kwa wafanyakazi wanapokuwa katika majukumu yao.
Akizungumza mara baada ya ugawaji wa tuzo hiyo, Rais wa TOHASA Caroline Baraza aliipongeza EACOP kwa kutwaa tuzo hiyo, ambayo pia ilikuwa inashindaniwa na makampuni/mashirika/taasisi mbalimbali .
“Katika mchakato wa kupata mshindi kwenye tuzo hii tulizingatia sifa kadhaa, kuu zikiwa namna ya kusimamia usalama wa wafanyakazi na kuzingatia afya zao, ambazo kwa kiasi kikubwa zimeufanya mradi huu kushinda tuzo hii”, alisema Baraza.
Kwa mujibu wa Baraza, baadhi ya wafanyakazi wamekuwa wapoteza maisha katika sehemu zao za kazi kwa kutofuata sheria za usalama mahali pa kazi, ikiwemo wamiliki wa viwanda, migodi au wajenzi kutolipa umuhimu suala hili kwa kutoa elimu ya usalama mara kwa mara na kushindwa kuzuia ajali zinazoweza kutokea.
“Pamoja na sababu nyingine , kilichopelekea EACOP kuibuka mshindi wa tuzo hii ni usimamizi mzuri wa utekelezaji wa sheria ya kusimamia usalama kazini kupitia kampeni yao iitwayo ‘zero harm’, ikimaanisha hakuna madhara mahali pa kazi kwa wafanyakazi wake” alibainisha Bi Baraza.
Aidha, Baraza alisema kuwa mwamko kwa sasa katika jamii kuhusu umuhimu wa kuzingatia usalama sehemu ya kazi umeongezeka kwa kiasi kikubwa kupitia tuzo hizi na elimu mbalimbali kutolewa.
“Lengo ni kuhamaisha kila sehemu ya kazi kuona umuhimu wa kuzingatia sheria na hatua zote za usalama na afya kwa wafanyakazi na watumishi wengine katika sehemu zote za kazi,”
“Kuna baadhi wa wafanyakazi wanafanya kazi hatarishi , hivyo ni vema viongozi na wasimamizi wakazingatia usalama wao, ikiwemo kutoa elimu za mara kwa mara kwa wafanyakazi wao na kuwapa vifaa kinga, kutegemeana na aina ya kazi wanazofanya,” alisema.
Mbali na kushinda tuzo hiyo, Baraza pia aliusifu mradi wa EACOP kwa kuwajali wafanyakazi wake na kusaidia ufadhili wa zaidi ya wanafunzi 50 kutoka vyuo vikuu mbalimbali hapa nchini kwa ajili ya kujifunza masuala ya afya na usalama kazini.
Naye Meneja wa Afya na Usalama kazini wa EACOP, Stacy Bridgewater aliishukuru TAHOSA kwa kutoa tuzo hiyo na kwa kutambua jitihada za mradi huo za kusimamia afya na usalama katika maeneo ya kazi.
“Tumeweza kuajiri takriban watu 8,000 kutoka ndani na nje ya nchi waliopo katika makambi mbalimbali hapa nchini kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu,”
“Hivyo, suala la afya na usalama wao ni kipaumbele chetu, tena tunasimamia kwa uangalifu mkubwa na hatutaki kuona mtu anapata madhara yoyote akiwa kazini,”
Alisema kwa wafanyakazi waliopo katika maeneo ya ujenzi, uvaaji wa vifaa vya kulinda usalama wao (PPE) ni lazima wakati wote ikiwemo uvaaji wa kofia ngumu, hata wageni wanaotembelea maeneo haya wanalazimika kuvaa vifaa kinga.
“ Kuna alama za kutosha ndani ya maeneo ya mradi kwa ajili ya kusisitiza juu ya usalama wa kila mmoja na tumeweka utaratibu kwa kila mtu kuweza kutoa taarifa ya kitu chochote anachohisi kinaweza kuwa ni hatarishi,” amesema
Mradi wa EACOP una urefu wa kilomita 1, 443 kutoka Hoima nchini Uganda mpaka Peninsula ya Congoleani mkoani Tanga kwa ajili ya kusafirisha mafuta hayo kwenda katika soko la kimataifa.
Washirika wa mradi wa EACOP ni Total energies ikiwa na asilimia 62, Shirika la Maendeleo la Mafuta nchini (TPDC) na Kampuni ya Mafuta ya nchini Uganda (UNOC) ambazo kila moja inamiliki asilimia 15 pamoja na Kampuni ya kitaifa ya Mafuta ya China (CNOOC) yenye hisa asilimia 8.
No comments:
Post a Comment