FILAMU YA AMAZING TANZANIA NA ROYAL TOUR YAFUNGUA SOKO LA UWINDAJI WA KITALII KWA WAWEKEZAJI KUTOKA CHINA - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Friday, February 21, 2025

FILAMU YA AMAZING TANZANIA NA ROYAL TOUR YAFUNGUA SOKO LA UWINDAJI WA KITALII KWA WAWEKEZAJI KUTOKA CHINA


NA JOYCE NDUNGURU

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) amesema jitihada za Serikali zilizofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kutangaza utalii kupitia filamu za Royal Tour na Amazing Tanzania zimefungua soko la uwindaji wa kitalii Nchini China.

Ameyasema hayo leo tarehe 21 Februari, 2025, katika Chuo cha  Utalii cha Taifa (NCT) jijini Dar es Salaam kwenye Hafla ya kukabidhi vyeti vya umiliki wa vitalu vya uwindaji wa kitalii kwa wawekezaji mbalimbali kutoka Makampuni ya K&F Wild  Expedition Limited, Michael Mantheakis Safaris Limited, Out of Africa Safaris Limited na Royal Conservation Limited.


"Nichukue fursa hii kuwapongeza makampuni yote kwa kushinda vitalu hivi vya uwindaji wa kitalii sambamba na hilo  nichukue fursa hii kumpongeza mwekezaji kutoka Nchini China kwa kupitia kampuni ya K&F Wild Expedition Ltd kwa kuwa kampuni ya kwanza ya kutoka China kuwekeza katika vitalu vya uwindaji wa kitalii nchini," amesema Mhe. Chana.


Ameongeza kuwa soko la uwindaji wa kitalii nchini China linakua kwa kasi na yote haya ni kwa kupitia jitihada zinazofanywa na Serikali za kutangaza utalii duniani.


Sambamba na utoaji wa vyeti kwa wawekezaji, Chana alishuhudia zoezi la utiaji saini mikataba ya uwekezaji mahiri (Special Wildlife Investment Concessions Areas- SWICA) kati ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) na Kampuni ya Neon Investment Limited.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TAWA, Mej. Jen (Mstaafu) Hamis Semfuko amesema kuwa TAWA inaendelea kutumia mbinu mbalimbali za kuvutia wawekezaji ikijumuisha matumizi ya mnada wa kielektroniki wa ugawaji wa vitalu.


Sanjari na hilo, Mej.Jen (Mstaafu) Semfuko ameongeza kuwa Bodi ya Wakurugenzi  itaendelea kutafuta masoko mengine ya uwindaji wa kitalii yakiwemo nchi za China, Urusi, Uturuki, Brazil na Mashariki ya Mbali ili kuhakikisha wawekezaji wanaongezeka na Nchi inaendelea kupata mapato.


Naye, Kaimu Kamishna wa TAWA Mlage Kabange, amesema kupitia uwekezaji huu Serikali inatarajia kupokea mapato na tozo mbalimbali. 


"Kupitia ada za vitalu za makampuni haya Serikali inatarajia kupata mapato takribani shilingi za kitanzania Bilioni 2.5 kwa mwaka mbali na kodi nyingine."


Sambamba na hilo, Kaimu Kamishna Kabange amesema kuwa uwekezaji huu unawagusa pia wananchi wanaoishi pembezoni ya hifadhi kwa kuzingatia kuwa kwenye mikataba hii kuna kipengela mahsusi cha kunufaisha jamii zinazoishi pembeni mwa hifadhi.






No comments:

Post a Comment