TANZANIA YAVUTIA WAWEKEZAJI KUPITIA MKUTANO WA BIASHARA NA UWEKEZAJI MARSEILLE - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Thursday, February 20, 2025

TANZANIA YAVUTIA WAWEKEZAJI KUPITIA MKUTANO WA BIASHARA NA UWEKEZAJI MARSEILLE


NA MWANDISHI WETU, UFARANSA

MKUTANO wa Biashara na Uwekezaji (Business and Investment Forum) uliofanyika kwa siku mbili Marseille, Ufaransa 11-12 Februari 2025 umefungua fursa mpya kwa Tanzania katika kuvutia wawekezaji wa kimataifa. 


Ujumbe rasmi kutoka Tanzania, ukiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya  Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC), David Kafulila, ulihudhuria mkutano huo wenye lengo la kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Ufaransa.

Katika mkutano huo uliofunguliwa rasmi na Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania,  Ali Jabir Mwadini, ambaye alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kibiashara kati ya mataifa haya mawili. Katika hotuba yake, alibainisha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye fursa kubwa za uwekezaji barani Afrika, hasa katika sekta za kilimo, utalii, miundombinu, na nishati.


Katika mijadala iliyofanyika, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kilitoa wasilisho maalum likielezea fursa mbalimbali zinazopatikana nchini Tanzania, huku likitoa mwanga kwa wawekezaji kuhusu mazingira wezeshi ya biashara. Ujumbe wa Tanzania pia ulihusisha wawakilishi kutoka Wizara ya Kilimo, Ofisi ya Rais, Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), pamoja na Sekta ya Utalii.


Mbali na majadiliano ya kitaalamu, washiriki wa mkutano walipata nafasi ya kushiriki katika shughuli za mtandao (networking), ambapo wawekezaji wa kimataifa walipata fursa ya kujadili uwezekano wa kushirikiana na sekta mbalimbali nchini Tanzania.


Mkutano huo ulimalizika kwa ziara ya kutembelea kiwanda cha CMA kilichopo Ufaransa, ambapo wajumbe wa Tanzania walipata nafasi ya kujifunza mbinu za kisasa za uzalishaji viwandani


Mkutano wa Biashara na Uwekezaji wa Marseille umedhihirisha dhamira ya Tanzania katika kujenga ushirikiano imara na mataifa ya Ulaya, huku ukifungua njia kwa wawekezaji zaidi kuchangamkia fursa zilizopo nchini.





No comments:

Post a Comment