NA MWANDISHI WETU
CHAMA Cha Wananchi (CUF) kimesikitishwa na matukio inayodai yamekuwa ni ya kujirudia kwenye jamii ikiwemo kutekwa, kuteswa na hata kuuawa na watu wanaodaiwa wasiojulikana.
Katika taarifa iliyotolewa leo na kitengo cha Uenezi na Mawasiliano ya Umma ya chama hicho na kusainiwa na Mkurugenzi wake Injinia Mohamed Ngulangwa, imesema tukio linatoa ikiwa ni miezi tisa tangu aliposhushwa garini na baadae kuripotiwa kuuawa, aliyekuwa kiongozi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Ali Kibao.
"Wakati huo ilikuwa ni kipindi cha 'mshike mshike' kuelekea kwenye Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa chama hicho na sasa tunapokea kwa huzuni na mshtuko mkubwa taarifa ya kushambuliwa kwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki (TEC), Padri Charles Kitime na kuumizwa vibaya,"
"Kwa vyovyote vile bila kujali nani anatekeleza uharamia huu, tunalaani vikali mfululizo wa matukio ya aina hii na Watanzania tunafarijika pale majeshi yetu, hususan Jeshi la Polisi, yanapojitokeza mbele ya umma kudhihirisha kuimarika kwake kiweledi na kwa vifaa madhubuti katika kupambana na uhalifu na mbinu bora za kisasa za uchunguzi na upelelezi," imesema.
Aidha taarifa hiyo imebainisha kuwa CUF, inatoa wito kwa Serikali chini ya Dkt Samia Suluhu Hassan kukomesha haraka matukio ya aina hiyo, kwani watanzania wanatarajia kusikia angalau taarifa za awali zinazohusu uchunguzi kuhusu kadhia za utekaji, utesaji na mauaji yanayoongeza taharuki kila uchao.
Pia CUF inatoa Pole kwa Padri Kitime na wale wote wanaokutwa na matukio hayo na kuwaombea wapone haraka na kurudi kwenye majukumu yao.





No comments:
Post a Comment