MSAJILI WA HAZINA ATOA TASWIRA MPYA - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Monday, June 2, 2025

MSAJILI WA HAZINA ATOA TASWIRA MPYA


 NA MWANDISHI WETU

Katika hatua inayoonesha mafanikio ya mageuzi makubwa ndani ya taasisi za umma, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, ametangaza ongezeko kubwa la mapato yasiyo ya kodi, yakifikia Shilingi bilioni 884.7 ndani ya miezi 11 ya mwaka wa fedha 2024/25. Hili ni ongezeko la asilimia 40 kutoka bilioni 633.3 zilizokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka uliopita.


Kwa mujibu wa Mchechu, mafanikio haya yametokana na usimamizi madhubuti wa mali za umma, matumizi sahihi ya mifumo ya TEHAMA, pamoja na mabadiliko ya kifikra katika uendeshaji wa mashirika ya umma na kampuni ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache.


 "Leo hii tunazungumza juu ya taasisi na mashirika 258 yaliyosajiliwa, 201 kati yao tumeweza kuyafikia kwa karibu na tayari tumeweka misingi ya usimamizi wa pamoja kupitia mifumo iliyounganishwa," alisema Mchechu akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam.


MAGEUZI YA KIFIKRA YENYE TIJA

Katika kipindi cha miaka miwili tu, Ofisi ya Msajili wa Hazina imefanikiwa kuunganisha taasisi 14, kuunda taasisi mpya sita, na kuzifuta taasisi tatu zisizokuwa na tija. Aidha, taasisi 57 zimewezeshwa kujiendesha kwa uhuru baada ya maboresho ya kimuundo na kiutendaji.



Katika kuhakikisha utendaji unaleta tija kwa taifa, ofisi hiyo pia imefanikiwa kuongeza mtaji wa Benki ya TCB kwa Shilingi bilioni 131, hatua iliyoiwezesha benki hiyo kutengeneza faida ya Shilingi bilioni 31.6 mwaka 2024. Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pia limeonesha mafanikio makubwa, ambapo faida imeongezeka kutoka Shilingi bilioni 0.9 hadi bilioni 21.8 katika mwaka huo huo.


MIFUMO YA KISASA YANYANYUA MAPATO

Ufanisi huu mkubwa umetokana na matumizi ya mifumo iliyounganishwa kama PlanRep, ERMS, e-Watumishi na MUSE. Kwa kutumia teknolojia, ofisi imeweza kufuatilia mwenendo wa kifedha wa taasisi zote kwa wakati halisi, hivyo kuondoa mianya ya upotevu wa mapato.


Gawio kutoka kwa mashirika ya umma limechangia asilimia 63.9 ya mapato yote, huku michango ya asilimia 15 ya mapato ghafi ikichangia asilimia 29.7, na mapato mengineyo yakiwa asilimia 6.4.


THAMANI YA UWEKEZAJI YAPANDA

Thamani ya uwekezaji wa serikali katika taasisi na kampuni ambamo ina hisa imeongezeka kutoka Shilingi trilioni 75.79 mwaka 2022/23 hadi kufikia Shilingi trilioni 86.29 mwaka 2023/24. Hii inaashiria kuwa mali za umma si tu zimehifadhiwa, bali zimeongezewa thamani kwa ustadi wa kitaalamu na ufuatiliaji wa karibu.


SIRI YA MAFANIKIO: MAONO YA RAIS SAMIA

Mchechu amemsifu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa maono yake makubwa ya mageuzi na uboreshaji wa taasisi za umma. Kwa mujibu wake, mafanikio haya hayawezi kutenganishwa na msukumo wa kisera na maelekezo ya Mheshimiwa Rais kuhusu ufanisi, uwajibikaji, na thamani ya fedha kwa kila kitendo cha serikali.


"Siku ya Gawio mwaka huu ni zaidi ya tukio la kifedha. Ni alama ya uwajibikaji wa pamoja na tathmini ya namna mashirika yetu yanavyofanikisha malengo ya taifa. Lengo letu ni kufikisha trilioni 1 – na tuna imani tutavuka lengo hilo," alieleza Mchechu.


Siku ya Gawio ya mwaka huu inatarajiwa kufanyika Juni 10, 2025, ambapo mashirika yote yanayomilikiwa na serikali yanatakiwa kuwasilisha gawio lao kwa serikali. Tayari msisitizo umetolewa kwa taasisi ambazo hazijatimiza wajibu huu kufanya hivyo kabla ya tarehe hiyo.

No comments:

Post a Comment