WAZIRI MHAGAMA AWEKA BAYANA MAENDELEO SEKTA YA AFYA SIMIYU - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Wednesday, June 18, 2025

WAZIRI MHAGAMA AWEKA BAYANA MAENDELEO SEKTA YA AFYA SIMIYU


NA WAF, SIMIYU


WAZIRI wa Afya Jenista Mhagama ameyataja maboresho makubwa ya huduma za afya katika mkoa wa Simiyu ambayo yameletwa chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.


Amesema hayo leo Juni 18, 2025 alipopata fursa ya kuzungumza na halaiki ya wananchi waliojitokeza kwenye mkutano wa hadhara wa Mhe. Rais Dkt. Samia ulifanyika stendi ya zamani Bariadi, Simiyu. 


“Sekta ya Afya ni ulinzi na uhai kwa wananchi wa Tanzania, tunakushukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuipa kipaumbele Sekta ya Afya na kuboresha huduma za afya kwa wwnanchi,” amesema Waziri Mhagama.


Waziri Mhagama amesema jitihada za Rais Samia katika kuwekeza kwenye huduma za afya ya uzazi mama na mtoto zimechangia katika kupungua kwa idadi ya vifo vitokanavyo na uzazi kutoka vifo 556 hadi 104 kwa vizazi hai 100,000 huku akijata takwimu za mkoa wa Simiyu kuwa vifo kwa sasa ni 33 kwa kila vizazi hai 100,000.


Amesema kuwa Serikal imetoa kiasi cha Shilingi Bilioni 7.4 kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya mama na mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu.


“Rais Samia alipoona kuna changamoto ya huduma za afya ya uzazi mama na mtoto alitoa Shillingi Bilioni 7.4  kwa ajili ya kujenga wodi maalum ya akina mama kujifungua katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu, asante Rais Samia kwa kutuhakikishia usalama wa watoto na uhai kwa wanawake wa Tanzania kupata huduma bora za afya ya uzazi,” ameeleza Waziri Mhagama.


Waziri Mhagama amesema kuwa baada ya uboreshaji wa huduma za afya ya uzazi Rais Samia ameona bado kuna haja ya kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya kwa watoto wachanga njiti pamoja na wale wenye uhitaji wa huduma za kibingwa ambapo Rais Samia ameelekeza Shilingi Bilioni 4.59 ziletwe Simiyu kabla ya mwezi wa kumi kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya kutolea huduma.


Ameeleza uwekezaji mkubwa wa Sekta ya Afya katika mkoa wa Simiyu umerahisisha upatikanaji wa huduma za kibingwa na hivi sasa rufaa za matibabu ikiwemo huduma za uchunguzi kupitia mashine za CT-Scan umepungua kutoka rufaa 400 hadi kufikia rufaa 150.


“Mhe. Rais umewezesha upatikanaji wa Digital Xray mashine nchi nzima na hapa katika mkoa wa Simiyu zinapatikana hadi kwenye Hospitali za Halamshauri za Wilaya sita (6) katika mkoa wa Simiyu,” amesema Waziri Mhagama akimshukuru Rais Samia kwa kuwekeza kwenye huduma za Radiolojia.


Kuhusu upatikajani wa hewatiba ya oksojeni, Waziri Mhagama amesema kuwa Serikali imetoa zaidi ya Shilingi Bilioni 1.8 kwa ajili ya ujenzi na usimikaji ma mashine za uzalishaji ambapo tayari ujenzi umeshaanza.

No comments:

Post a Comment