NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Viwanda na Biashara Dkt Selemani Jaffo, anatarajia kuwa mgeni rasmi katika Maonesho ya pili ya Huduma za Kifedha na Kijamii 'Muharram Expo' yanayoendelea katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Kiongozi Mwandamizi wa Taasisi za Kiislamu Tanzania, Mohamed Issa, maonesho hayo ni ishara ya kuingia mwaka mpya wa Kiislamu ambao ni Muharram.
"Maonesho haya ambayo yameanza Jumanne wiki hii na yatahitimishwa baada ya siku saba yanajumuisha shughuli mbalimbiali za kifedha zisizo za riba kama bila huduma za kibenki, vicoba na Saccos," amesema.
Aidha amesema kuwa katika maonesho hayo wananchi watakaofika kujionea shughuli hizo watapata fursa ya kupata elimu ya namna ya kuweka akiba, kupata mikopo au uwezeshwaji usio na riba.
Pia amesema wananchi watapewa elimu kuhusu huduma za Masoko ya mitaji na dhamana na uwekezaji wa pamoja (Collective Investment Schemes) isiyo na riba kama vile mifuko ya Uwekezaji Halal au Halal Fund, hati fungani zisizo na riba inayofahamika kama Sukuk.
Vile vile watapewa elimu kuhusu hisa za kampuni, zilizokidhi masharti ya Shari'ah hivyo kuwa Halal na namna ya kujichunga na hisa zisizo Halal, pia watapewa huduma za kifedha na maelezo ya huduma za kijamii kama vile uwekaji wa wakfu, huduma za afya kutoka kwa jopo la madaktari.
Katika maonesho hayo zitawasilishwa mada za uchumi na fedha na kufahamu madhara ya riba, mada hizo zitakuza uelewa kwa jamii kuhusu masuala ya uchumi.
Naye Amiri wa Baraza Kuu la Kiislamu, Sheikh Mussa Kundecha, amebainisha kuwa maonesho hayo si kwaajili wa waislamu pekee bali ni kwa Watanzania wote bila kujali dini.
"Ndio maana tumeyaweka katika viwanja vya wazi ili kila mwananchi afike kupata huduma hususan wafanyabiashara ambao wameathirika na mikopo ya kausha damu hivyo watapata elimu sahihi kuhusu mikopo," amesema.
Pia alisema katika maonesho hayo kutakuwepo uchangiaji wa damu, huduma za msaada wa kisheria kuhusu masuala ya kisheria.
No comments:
Post a Comment