SHILINGI BILIONI 161.3 KUIMARISHA HUDUMA ZA AFYA MSINGI NCHINI - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Saturday, July 19, 2025

SHILINGI BILIONI 161.3 KUIMARISHA HUDUMA ZA AFYA MSINGI NCHINI

NA WAF

SERIKALI imeazimia kutumia Shilingi Bilioni 161. 3 za Mfuko wa pamoja wa Afya kwa ajili ya kuboresha na kuimarisha mifumo ya afya nchini ili kutoa huduma bora za afya ya msingi kwa wananchi sambamba na kupunguza vifo vya watoto vitokanavyo na uzazi na kuimarisha huduma za bima ya afya kwa wote. 


Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Afya  Jenista Mhagama, Julai 18, 2025, Jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kusaini makubaliano  (Side Agreement) kwa mwaka wa fedha 2025/26 baina ya Serikali ya Tanzania na Wadau wake tisa (9) wa Maendeleo wanaounga mkono Mfuko wa Pamoja wa Afya (Health Basket Fund - HBF) – ambao ni Canada, Denmark, Ireland, Korea Kusini, Uswisi, Uingereza, UNFPA na UNICEF. 


Amesema wadau wa maendeleo wameahidi kutoa jumla ya Dola za Kimarekani Milioni 55.9 sawa na takribani Shilingi Bilioni 161.3 za Kitanzania kwa mwaka wa fedha 2025/26, fedha ambazo zitatumika kugharamia ununuzi wa dawa, vifaa tiba, na vifaa vya afya pamoja na kuimarisha mifumo ya utoaji wa huduma bora za afya ya msingi, vituo vya afya, mikoa hadi ngazi ya taifa.


“Wadau wetu wa maendeleo wameridhishwa na kuimarika kwa huduma za afya ya mama na mtoto na hatua ya kuanzisha  kwa Bima ya Afya kwa Wote, sasa tunakwenda   kuongeza nguvu zaidi katika kudhibiti vifo vya watoto vitokanavyo na uzazi,” amesema Waziri Mhagama.


Waziri Mhagama amesema kupitia mipango, mikakati na vipaumbele vinavyowekwa na Serikali ya Tanzania katika matumizi madhubuti ya fedha ndio imekuwa chachu na kivutio kwa wadau kuongeza fedha za miradi ya maendeleo.


“Serikali ya Tanzania inasimamia vizuri mipango na mikakati tunayopanga na wadau wetu, wanatupongeza kwa sababu ya utendaji kazi mzuri wa kusimamia fedha hizi na kwa hilo nitumie fursa hii kuwapongeza watendaji wetu kwa usimamizi madhubuti wa fedha hizi," amesema Waziri Mhagama.


Aidha Waziri Mhagama amewaagiza makatibu wakuu wa wizara zinazoigusa sekta ya afya kuhakikisha  kamati   za kitaalam   zinafanya kazi na kutatua  changamoto zinazojitokeza wakati wa utekelezaji kwa kuzingatia maeneo yote muhimu na kuwashirikisha mawaziri husika kwa hatua zaidi.


Tangu kuanzishwa mfuko huo mwaka 1999, zaidi ya Dola za Kimarekani Bilioni 1.3 sawa na takribani Shilingi Trilioni 3.2 zimeshatolewa kwa ajili ya kutekeleza Mipango  Mkakati ya Sekta ya Afya.


Aidha kuanzia mwaka 2017, fedha zimekuwa zikipelekwa moja kwa moja kwenye vituo vya afya vya umma  na zaidi ya vituo vya afya vya ngazi ya msingi 7,300 vimenufaika na fedha hizo.






No comments:

Post a Comment