NA MWANDISHI WETU
WAKULIMA wa mbogamboga, matunda, viungo na vikolezi, wameshauriwa kwenda Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI Tengeru), kujifunza teknolojia nzuri za kilimo hicho.
Mwito huo ulitolewa mwishoni mwa wiki na Kaimu Meneja wa TARI Tengeru, Dk Happiness Mollel akizungumza na mwandishi wa habari hizi, mkoani Dar es Salaam.
Alisema TARI Tengeru imejikita katika kutafiti mbegu za mbogamboga, matunda, viungo na vikolezi, hivyo iwapo wakulima wa bidhaa hizo watatumia vema elimu watakayopewa wataongeza tija ya uzalishaji.
“TARI Tengeru tuna teknolojia za kuzalisha mbegu za mchicha, ngogwe, nyanya na figiri. Pia tunaongeza thamani kwenye mazao yetu; tunatengeneza unga lishe kupitia mahindi ya njano, mchicha nafaka na uwele, mchicha nafaka una protini nyingi, hivyo mtu akinywa uji wa mchanganyiko huo atafaidika,” alisema.
Dk Happiness alisema pia wameongezea thamani kwenye tunda la mizizi ya beet kutoka kutengeneza sharubati na kula lilivyo hadi kupata mvinyo.
Kaimu Meneja huyo alisema kupitia TARI Tengeru, wameongeza thamani kwenye viungo kama nyanya zenye soko la uhakika.
Pia, alisema wamefanya utafiti wa mbegu bora za mchicha zinazotumia muda mfupi kuzaa, hivyo kumhakikishia mkulima kipato cha uhakika kwa muda mfupi.
“Ili kuweza kulima mbogamboga, unapaswa kujua afya ya udongo wako una rutuba kiasi gani, mbegu sahihi zinazotoka kwenye taasisi zilizothibitishwa na Mamlaka husika, kama Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) na TARI,” alisema.
Alisema TARI kwa sasa ina mbegu za mchicha ukiwamo mchicha pori, akeri (mchicha nafaka), nguruma (mchicha bwasi) unaovunwa kwa muda mrefu.
Alisema pia wanazalisha mbegu za nyanya Tenguru 97, tanya, cheri na nyingine, huku akisisitiza kuwa mbegu zao zina ubora kwa kuwa zimepitia Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), ili kupata uthibitisho.
Dk Happoness alisema kutokana na uwekezaji wa kituo hicho kupitia mashamba darasa, wamezalisha tani mbili za mbegu za mbogamboga.
Mtafiti Mwandamizi wa TARI Tengeru, Emmanuel Lasway alisema ili mkulima wa mbogamboga afanikiwe, anapaswa kufuata taratibu za kiagromia, ambazo ni shamba lenye udongo usiotuamisha maji na maji ya kumwagilia.
Lasway alisema pia mkulima anapaswa kutumia udogno kutoka kwenye msitu, kutengeneza kitalu kinachotumia mbegu chache na baada ya hapo miche ihamishwe shambani.
“Mkulima anapaswa kumwagilia mbegu hadi ziwe na urefu wa sentimeta tano hadi 10, huku maandalizi ya shamba yakiwa tayari na kuhakikisha umwagiliaji unakuwa mzuri muda wote,” alisema.
Alisema upandaji bamia matuta yanatakiwa kuwa na umbali wa sentimeta 60, mche na mche sentimeta 45, lakini mchicha, mnavu na pilipili umbali ni sentimeta 30, huku akitaka wakulima kuandaa mbolea ya kuoteshea ambayo inawekwa gramu tano kila shina baada ya kuchanganya na udongo.
Alisema ili kupata mavuno mazuri baada ya wiki mbili, mkulima anapaswa kuweka gramu tano hadi 10 ya mbolea yenye kiwango kikubwa cha nitrojeni.
“Jambo la kuzingatia katika kilimo cha mbogamboga ni kuhakikisha maji ya kumwagilia yanakuwa ya kutosha, kudhibiti visumbufu na kuhakikisha hakuna magugu,”alisema.
No comments:
Post a Comment