Mkuu wa Takukuru mkoani Pwani, Domina Mkama akizungumza katika semina hiyo.
NA MWANDISHI WETU, PWANI
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Pwani imetoa mafunzo kwa Waandishi wa Habari, Viongozi wa Dini na Asasi za Kiraia kwaajili ya kuzuia vitendo vya rushwa katika kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Katika semina hiyo ambayo imefanyika leo Agosti 28, 2025 mkoani humo, Mkuu wa Takukuru mkoani Pwani, Domina Mkama, wakati anafungua semina hiyo aliyasisitiza makundi hayo kuhakikisha wanatoa elimu ya kuzuia na kupambana na rushwa ili kupata viongozi wasiotokana na rushwa.
“Viongozi wa dini mtusaidie kutoa elimu kwa jamii mnayokutana nayo, tunaamini mkisema chochote kupitia maneno ya dini kinafika kwa haraka, kwetu sisi tunaangalia zaidi sheria hivyo tukiunganisha nguvu tutafanikiwa hususan katika kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu.
“ Pia Azaki za kiraia, Waandishi wa Habari kwa nafasi zenu mnawajibu wa kuelimisha umma kwani masuala ya rushwa yanaathiri maendeleo katika jamii hususan kiuchumi, wote twende na kauli mbiu yetu inayosema “ Kuzuia Rushwa ni Jukumu Lako na Langu Tutimize Wajibu wetu”, amesema.
Baadhi ya viongozi wa dini ambao amepata nafasi ya kushiriki katika semina hiyo akiwemo Sheikh wa Mkoa wa Pwani, Abbas Mtupa alitoa wito kwa taasisi hiyo kuendelea kutoa mafunzo ya aina hiyo kwa makundi hayo mara kwa mara jambo litakalosaidia kuwa karibu na jamii zaidi.
“Pia naomba Takukuru mjishushe kwa jamii ya chini kabisa, hii itasaidia mchakato wa kuzuia na kupambana na rushwa kuwa rahisi na mapambano haya yameelekezwa katika vitabu vya dini kwa tasfiri yake mnafanya kazi nzuri na anayeshiriki kwenye rushwa amelaaniwa na Mungu,” amesema.
Katika semina hiyo mada tatu zilitolewa ambazo ni namna ya Kuzuia Vitendo Vya Rushwa Katika Uchaguzi, Madhara ya Rushwa Katika Uchaguzi na Sheria Za Uchaguzi.
![]() Mkuu wa Dawati la Uchunguzi wa Takukuru mkoani Pwani, Juliana Bulinda akitoa mada kuhusu Madhara ya Rushwa Katika Uchaguzi |

Mwanasheria wa Takukuru mkoani Pwani, Leonard Swai, akitoa mada kuhusu Sheria za Uchaguzi.
No comments:
Post a Comment