WORLD VEGETABLE CENTRE KUENDELEA KUFANYA TAFITI KUPATA MBEGU BORA - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Friday, August 15, 2025

WORLD VEGETABLE CENTRE KUENDELEA KUFANYA TAFITI KUPATA MBEGU BORA


NA MWANDISHI WETU, ARUSHA 

 TAASISI ya Kimataifa ya Utafiti na Uendelezaji wa Kilimo cha Mbogamboga Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika ‘World Vegetable Centre’ iliyopo Tengeru mkoani Arusha imesema  itaendelea kufanya utafiti ili kuzalisha mbegu bora zinazoweza kustahimili ukame, magonjwa, na mabadiliko ya tabianchi.


Aidha, taasisi hiyo imesema lengo la utafiti ni kuongeza usalama wa chakula na kipato kwa wakulima.


Kwa kushirikiana na taasisi nyingine za utafiti wa kilimo kama Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini (TARI) na Mamlaka ya Afya ya Mimea nchini (TPHPA) ,WorldVeg kwa kutumiwa wataalamu wake na maabara za kisasa inasambaza zaidi ya sampuli 10,000 za mbegu kutoka katika benki yake ya mbegu kwa wanasayansi, wakulima na taasisi mbalimbali za kilimo kwa ajili ya kuzifanyia utafiti na kuziboresha kwa matumizi ya kilimo.



Akizungumza wakati wa mafunzo ya siku tatu ya nadharia na vitendo  ya utunzaji wa mbegu, kuanzia uhifadhi wa vinasaba vya mimea, ukaushaji na namna ya kupima uwezo wa mbegu hizo kuota katika maabara yake ya kisasa kati kati ya wiki, Bw. Abdul Shango, Mtaalamu wa Mbegu na Mtafiti taasisi hiyo amesema wameweza kufanya tafiti ya mbegu hizo zinazotumika katika nchi mbalimbali barani Afrika na matokeo yake yamekuwa na matokeo chanya.


“Tunatambua kuwa mabadiliko ya tabia nchi na ukosefu wa mvua katika maeneo mengi ni moja ya kikwazo katika ukuaji wa sekta ya kilimo barani Afrika,”


“Lakini pia ukosefu wa mbegu bora zinazoathiriwa na wadudu na hali ya hewa ni moja ya kikwazo na ndiyo maana tunatafanya tafiti na kuhifadhi aina mbalimbali za mbegu katika benki yetu zilizofanyiwa utafiti na baadae kuzisambaza kwa wakulima wadogo wadogo ili kukabiliana na changamoto wanazokumbana nazo ili kuza sekta hiyo hapa nchini,” amesema Shango.


Ameongeza kuwa mbegu hizo zinazalishwa kwa kutumia teknolojia za kisasa na kufanyiwa majaribio katika vitalu maalum ili kuhakikisha zinakidhi vigezo vya mazingira halisi ya wakulima.



 Chingnung Chiao, Msaidizi Mkuu wa Utafiti kutoka Makao Makuu ya World Vegetable Center yaliyopo nchini Taiwan aliyeendesha mafunzo hayo kwa watafiti wa kilimo hapa nchini juu ya mbinu bora za utambuzi wa mbegu zilizo hai na zilizokufa na namna ya uhifadhi wake alisema mafunzo hayo yana tija kwa wataalamu hao ili watumike katika uzalishaji.


“Tunajua wakati mwingine wakulima wanakuwa hawana uhakika kama mbegu wanazotumia zina ubora na kutoa mazao wanayoyatarajia wakati wa upandaji.


Kupitia mafunzo haya, tumewafundisha namna ya kutambua ubora wa mbegu, jinsi ya kutambua mbegu zilizo hai na zilizokufa na namna ya kuzifanya ziwe hai tena kwa kutumia vipimo vya maabara,” amesema Chingnung.


Alisisitiza kuwa mbegu bora ndizo msingi wa kilimo chenye tija na kwamba uelewa wa kisayansi kwa wakulima ni muhimu katika kubadilisha mfumo wa uzalishaji wa mbogamboga zinazotokana na mbegu za asili ya Afrika.


Kwa upande wake, Dkt. Judith Hubert, Mtaalamu wa Magonjwa ya Mimea kutoka katika taasisi hiyo ya Arusha alisisitiza umuhimu wa wakulima kutumia mbegu bora kama njia ya kukabiliana na changamoto za magonjwa na athari za mabadiliko ya tabia nchi.


“Tunawahamasisha wakulima kutumia mbegu bora zilizopimwa kisayansi, kwani ndizo zina uwezo wa kustahimili magonjwa na kuleta mavuno ya uhakika, tena kwa muda mfupi,”


“Vilevile, taasisi yetu inaendelea kutoa programu za uhamasishaji kwa wakulima ili wajifunze na kufaidika zaidi na mbegu hizi ambazo zinafanyiwa majaribio baada ya utafiti wa kisayansi kufanyika,” amesema.


Naye, Emmanuel Katamba, Mtafiti Msaidizi kutoka TARI amesisitiza kuwa utafiti wa kina wa mbegu ni chachu ya mafanikio katika sekta ya kilimo kwa kupata mazao bora yenye uhitaji sokoni.


“Tunapaswa kuendelea kuwekeza katika utafiti wa mbegu ili kuleta mageuzi katika kilimo. Mbegu bora ni chanzo cha mabadiliko chanya yakilimo chenye tija, kipato kwa wakulima, na uhakika wa chakula kwa taifa na dunia kwa ujumla,” amesema.


Amesema Tari inajivunia ushirikiano wake na taasisi hiyo ya Arusha katika kufanya tafiti ili kuendana na kasi ya ukuaji wa sekta ya kilimo duniani kwa kutumia mbinu na teknolojia ya kisasa.


No comments:

Post a Comment