NA MWANDISHI WETU,ARUSHA
SIKU chache baada ya aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango, kuzindua Makumbusho ya kisasa ya Jiopaki ya Ngorongoro-Lengai (Urithi Geo Museum) tarehe 16 Oktoba, 2025 wadau wameanza kuvutiwa na makumbusho hiyo na kuitembelea kwa lengo la kupata elimu kuhusu vivutio vya utalii, shughuli za uhifadhi wa maliasili na mambo kale.
Watalii na wadau wanaotembelea jengo hilo wanapata elimu kuhusu muonekano wa dunia miaka milioni mia mbili iliyopita na ilivyo sasa, maumbile asilia yanayopatikana katika ukanda wa bonde la ufa,kujionea mwamba wenye umri wa miaka milioni tatu iliyopita unaopatikana hifadhi ya Jiolojia ya Ngorongoro-Lengai, kujifunza tamaduni za makabila ya Wahadzabe, Wairaqw, Wadatoga na Wamasai pamoja, kupima uwezo wa kutambua sauti za wanyamapori, kushindana mbio kwa kutumia baiskeli na wanyamapori ndani ya makumbusho na vivutio vingine.
Miongoni wadau waliotembelea Makumbusho hiyo ni kundi la wanakwaya 22 wa KKKT Dayosisi ya kasikazini Jimbo la karatu usharika wa Qurus ambapo wametembelea jengo la Makumbusho kwa lengo la kujifunza vitu vilivyopo na kurekodi wimbo wa kwaya kwa ajili ya albam yao inayoitwa "Tumetoka mbali"
Kiongozi wa Kwaya hiyo Mwinjilisti Eliamani Kimay ameeleza kuwa kwaya hiyo kuamua kurekodi wimbo katika maeneo ya makumbusho hiyo ni kutokana na muonekano wa jengo hilo na maelezo ya vivutio vya utalii vilivyopo ndani ambapo kupitia kwaya hiyo wanatangaza injili kwa kutumia jengo hilo ambalo ndani yake kuna vioneshwa vya kipekee vinavyoashiria uumbaji wa Mungu
Mmoja wa wanakwaya wa kundi hilo Bi. Mariam Emmanuel ameeleza kuwa uamuzi wa kwaya yao kurekodi katika jengo hilo ni kuonesha vivutio vilivyopo Ngorongoro, kutangaza jengo hilo kupitia injili, kuonesha vivutio vilivyopo ndani ya makumbusho ili kuhamasisha wananchi wengi zaidi kupata elimu juu ya uumbaji wa Mungu, kufahamu masuala ya kijiolojia, urithi wa utamadani, malikale, historia ya chimbuko la binadamu ambayo kwa pamoja yanaashiria uumbaji wa Mungu.
Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ilipewa hadhi ya kuwa eneo lenye utalii wa Miamba “Geopark” mwaka 2018 na kuwa Jiopaki pekee katika nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara na ya pili kwa Afrika ikitanguliwa na Morocco.








No comments:
Post a Comment