WANUNUZI MADINI WILAYANI SAME WAONYWA - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Saturday, December 13, 2025

WANUNUZI MADINI WILAYANI SAME WAONYWA


NA MWANDISHI WETU

 SERIKALI kupitia Wizara ya Madini imewataka wanunuzi wa madini ya jasi yanayopatikana katika eneo la Makanya na Ruvu Jiungeni, wilayani Same mkoani Kilimanjaro, kuacha kupanga bei zao wenyewe na badala yake wazingatie bei elekezi zilizowekwa na serikali kupitia Tume ya Madini, Agizo hilo limetolewa baada ya kubainika uwepo wa  baadhi ya viwanda kujipangia bei ya ununuzi wa madini hayo, hali inayosababisha hasara kubwa kwa wachimbaji hao.


Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Dkt. Steven Kiruswa, wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za uchimbaji wa madini ya jasi wilayani Same, ambapo pia alizungumza na wachimbaji wadogo na kusisitiza umuhimu wa kurejesha mazingira kwa kufukia mashimo mara baada ya kukamilika kwa shughuli za uchimbaji.


Dkt. Kiruswa pia amebainisha fursa mbalimbali zilizopo kwa vijana na wanawake katika Sekta ya Madini kupitia programu ya Mining for a Brighter Tomorrow (MBT), akiwahimiza kuchangamkia mafunzo, upatikanaji wa leseni na matumizi ya vifaa vya kisasa ili kuongeza tija na usalama katika uchimbaji wa madini.


Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni amesema Serikali itaendelea kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sheria, kanuni na miongozo ya madini ili kuhakikisha wachimbaji wadogo na wananchi wa maeneo husika wananufaika na rasilimali hiyo kwa kukuza uchumi wao.


Naye Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Abel Madaha, amesema Tume ya Madini kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imekuwa ikifanya vikao mara kwa mara kutatua changamoto zinazowakabili wachimbaji kuanzia migodini hadi masoko ya madini.


Pamoja na hayo, Naibu Waziri wa Madini amesema Serikali inapanga kuwakutanisha wadau wa madini ya jasi mwanzoni mwa mwezi wa kwanza jijini Dodoma ili kujadili changamoto zinazowakabili wachimbaji wa Mkoa wa Kilimanjaro na kutafuta suluhu ya kudumu.


Kufuatia hatua hiyo imeibua furaha kwa upande wa wachimbaji wa madini hayo ambapo wameishukuru serikali kwa hatua wanazoendelea kuchukua ili kulinda maslahi ya wachimbaji huku wakieleza kuwa kikao hicho kitakachowakutanisha kitaleta mwafaka na suluhu za kudumu kwenye changamoto zao.

No comments:

Post a Comment