BILIONI 81/- KUMALIZA CHANGAMOTO YA MAJI MOROGORO - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Tuesday, January 20, 2026

BILIONI 81/- KUMALIZA CHANGAMOTO YA MAJI MOROGORO


 NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso (Mb), amesema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa Mtambo wa Kutibu Maji kutawezesha Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA) kuongeza uzalishaji wa maji kwa lita milioni 54 kwa siku.

Hiyo ni kutoka uwezo wa sasa wa kuzalisha lita milioni 47 kwa siku. Hatua hiyo itaifanya jumla ya uzalishaji wa maji kufikia lita milioni 101 kwa siku, ikilinganishwa na mahitaji ya sasa ya lita milioni 81.25 kwa siku, hali itakayotosheleza mahitaji ya maji ya Mji wa Morogoro kwa asilimia 100.


Waziri Aweso ametoa kauli hiyo wakati wa hafla ya utiaji saini wa Mkataba wa Uenzi wa Mtambo mpya wa Kutibu Maji-Mafiga wenye thamani ya takribani Shilingi Bilioni 81.41 ambao utazalisha lita Milioni 54 kwa siku ili kuboresha Huduma ya Majisafi katika Manispaa ya Morogoro.


Mradi huu, unaogharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Ufaransa kupitia Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), ni sehemu ya Mradi mkubwa wa Kuboresha Huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira wenye thamani ya takribani Sh. bilioni 200 ukiwa chini ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Morgoro (MORUWASA).


Akizungumza katika hafla hiyo Aweso amesema Serikali imedhamiria kumaliza kilio cha muda mrefu juu ya adha ya upatikanaji wa maji kwa kuhakikisha inatekeleza mradi mkubwa wa kutoa maji katika Bwawa la Mindu kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji kwa wakazi wa Manispaa ya Morogoro.


Waziri Aweso ameitaka MORUWASA kuhakikisha wanatumia utaalamu na uweledi wote walio nao kumsimamia Mkandarasi kutekeleza kazi hii katika ubora unaolingana na thamani ya fedha na kukamilika kwa wakati kama ulivyopangwa ili Wananchi wanufaike na uwekekezaji huo.


Aidha, Aweso ameahidi ushirikiano wa karibu na wadau wote wa Sekta ya Maji kwa dhumuni la kuendeleza kasi ya utendaji ili kuhakikisha mipango ya Serikali ya kuboresha huduma ya majisafi na usafi wa mazingira kwa Watanzania wote mijini na vijijini inatekelezwa kwa wakati na kwa viwango ili wananchi waweze kufikiwa na huduma iliyo bora ya majisafi na salama na yenye kutosheleza.





No comments:

Post a Comment