BRELA YATOA ELIMU KWA WANAFUNZI WA SHULE YA SEKONDARI FEZA BOYS - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Tuesday, February 17, 2026

BRELA YATOA ELIMU KWA WANAFUNZI WA SHULE YA SEKONDARI FEZA BOYS

 




NA MWANDISHI WETU

WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imetoa mafunzo kwa wanafunzi wanaosoma masomo ya biashara katika Shule ya Sekondari Feza Boys iliyopo Bahari Beach jijini Dar es Salaam.


Hatua hii inatokana na mabadiliko ya mtaala wa kufundishia ambao unawataka wanafunzi kusoma kwa nadharia na vitendo ikiwa ni pamoja na kupata elimu sahihi kutokana na uhalisia wake  kutoka taasisi husika.


Akizungumza wakati wa mafunzo hayo leo tarehe 17 Februari 2026, Afisa Usajili kutoka BRELA, Maryglory Mmary, alisema elimu hiyo inalenga kuwasaidia vijana kuelewa mapema taratibu za kisheria wakati wa kusajili biashara zao ili kuepuka changamoto wanapoingia katika shughuli za kibiashara baada ya masomo.


Aidha,  Mmary aliwaeleza kwa kina taratibu na vigezo vinavyohitajika katika kusajili majina ya biashara na kampuni huku akisisitiza umuhimu wa kufanya biashara kwa kufuata sheria na kanuni zilizopo ili kupata ulinzi wa kisheria na fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali.


Kwa upande wake Afisa Leseni, Lucas Mafuru, wakati akitoa elimu kuhusu umuhimu wa kuwa na Leseni ya Biashara Kundi A ambayo inatolewa na BRELA, aliwahimiza wanafunzi hao kuzingatia mamlaka husika kulingana na aina ya biashara wanayotaka kuanzisha.

“Ukitaka kuanzisha biashara au ukiwa na biashara ni muhimu kuwa na Leseni ya biashara ili uweze kukua na kuhimili ushindani wa soko, sisi BRELA tunatoa Leseni za biashara Kundi “A” ambazo hizi zina sura ya Kitaifa na Kimataifa lakini zile Kundi “B” zinatolewa na Halmashauri hivyo ni vyema kuzingatia mamlaka husika ukitaka kuanzisha au kufanya biashara,” alisema Mafuru.


Naye Afisa Sheria, Calvin Rwambogo, alitoa elimu kuhusu Alama za Biashara na Huduma, akiwaeleza kuwa hizi hutumika kutofautisha bidhaa au huduma za mfanyabiashara mmoja na mwingine sokoni na zinaweza kuwa katika mfumo wa nembo, alama au chapa (logo).


Aidha, Calvin aligusia pia suala la ulinzi wa Hataza ambapo alisema ili uvumbuzi upewe hati ya hataza ni lazima uwe mpya na usiotambulika kwa umma, usiwe rahisi kwa mtu mwingine kuutumia, uwe na mchango wa kutatua changamoto katika jamii, na usiwe na ufanano na uvumbuzi uliosajiliwa tayari.


Mafunzo hayo ya urasimishaji wa biashara ni sehemu ya mkakati wa BRELA wa kuwajengea vijana uelewa wa masuala ya biashara na haki miliki wakiwa bado shuleni, ili kuandaa kizazi cha wafanyabiashara wanaofuata sheria, wenye ubunifu na wanaochangia kikamilifu katika ukuaji wa uchumi wa taifa.







No comments:

Post a Comment