SERIKALI YATAKA HALMASHAURI KUPANGA BAJETI ZENYE MATOKEO, KUENDANA NA DIRA 2050 - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Tuesday, February 17, 2026

SERIKALI YATAKA HALMASHAURI KUPANGA BAJETI ZENYE MATOKEO, KUENDANA NA DIRA 2050


NA OWM TAMISEMI, DODOM

SERIKALI imezisisitiza halmashauri zote nchini kuandaa mipango na bajeti zinazozingatia matokeo, uwajibikaji na ufanisi, huku zikitekeleza vipaumbele vya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na Mpango wa Taifa wa Maendeleo.


Wito huo umetolewa leo Februari 17, 2026 Jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Bw. Sospeter Mtwale, wakati akifungua kikao kazi cha Makatibu Tawala Wasaidizi – Sehemu ya Mipango na Uratibu wa Mikoa pamoja na Wakuu wa Idara za Mipango na Uratibu wa Halmashauri zote Tanzania Bara.


Bw. Mtwale amesema ni muhimu kwa halmashauri kuhakikisha mipango na bajeti zao zinaendana na vipaumbele vya kitaifa ikiwemo Dira 2050, Mpango wa Taifa wa Maendeleo, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi na mipango mikakati ya maeneo husika.


Amesema kikao hicho kinafanyika katika kipindi ambacho Serikali ipo kwenye hatua za upangaji, uandaaji na utekelezaji wa mipango na bajeti kwa lengo la kuhakikisha matumizi bora ya rasilimali za umma na kuongeza tija katika utoaji wa huduma kwa wananchi.


Kwa upande wa utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano, Mtwale amesisitiza umuhimu wa uratibu madhubuti kati ya Serikali Kuu, Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri ili kuhakikisha mipango inayopangwa inaleta matokeo yanayoonekana kwa wananchi na kuchochea maendeleo ya uchumi wa maeneo.


Vilevile, amezitaka halmashauri kuzingatia tafiti na ubunifu katika upangaji wa mipango na bajeti kwa kuimarisha matumizi ya takwimu na ushahidi katika kufanya maamuzi.


“Nawasihi muendeleze utamaduni wa kufanya tafiti za kiutendaji, kubuni suluhisho za ndani kulingana na mazingira ya maeneo yenu na kutumia matokeo ya tafiti katika kufanya maamuzi ya mipango na bajeti ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa programu na miradi ya maendeleo,” amesema.





No comments:

Post a Comment