NA MWANDISHI WETU
Wataalamu kutoka Idara ya Misitu Zanzibar wamewasili katika Ofisi za Makao Makuu ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) jijini Dodoma kuanza ziara ya siku tano ya mafunzo katika Wilaya ya Manyoni, Singida, wakilenga kujifunza mfumo wa kisasa wa ufugaji nyuki unaotekelezwa na wakala huo.
Ujumbe huo unaoongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Misitu Zanzibar, Said Juma Ali, unajumuisha maafisa waandamizi watano na utakuwa nchini kuanzia Februari 11 hadi 15, 2026.
Imeelezwa kuwa ziara hiyo inalenga kuimarisha uelewa wa kitaalamu na uzoefu wa vitendo kwa watendaji wa Zanzibar hususan katika nyanja ya ufugaji nyuki endelevu, uanzishaji wa Hifadhi za Nyuki (Bee Reserves) na maendeleo ya Utalii wa Nyuki (Apitourism).
Akizungumza baada ya kuwasili, Said amesema Idara ya Misitu Zanzibar inapanga kuanzisha shughuli za utalii wa nyuki, shamba darasa la ufugaji nyuki na hifadhi maalum za nyuki, hivyo kuona umuhimu wa kujifunza kutoka TFS.
“Ziara yetu imelenga kuongeza uelewa na weledi katika ufugaji wa nyuki, hatua itakayochangia kuongeza kipato kwa jamii na kuimarisha uhifadhi wa bioanuai,” amesema.
Katika ziara hiyo, ujumbe huo unatarajiwa kujionea uendeshaji wa shamba darasa la nyuki la TFS Manyoni, mifumo ya kisasa ya uzalishaji wa asali, pamoja na usimamizi wa maeneo maalum ya nyuki yanayochangia uhifadhi wa misitu na rasilimali zake.
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi na Meneja wa Rasilimali za Nyuki wa TFS, Hussein Msuya, amesema TFS itaendelea kutoa elimu na kushirikiana na taasisi mbalimbali ili kuimarisha shughuli za ufugaji na maendeleo ya rasilimali za nyuki nchini.
Amesema ushirikiano huo ni sehemu ya juhudi za kitaifa za kuifanya sekta ya nyuki kuwa chanzo cha ajira, mapato na nyenzo muhimu katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.





No comments:
Post a Comment