MADIWANI MANISPAA YA KIBAHA WAPITISHA BAJETI YA 2026/2027 YA TSH BILIONI 68.7 KWA KISHINDO - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Wednesday, February 18, 2026

MADIWANI MANISPAA YA KIBAHA WAPITISHA BAJETI YA 2026/2027 YA TSH BILIONI 68.7 KWA KISHINDO


 NA MWANDISHI WETU

MADIWANI wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha mkoani Pwani wamepitisha kwa kishindo bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 yenye jumla ya Shilingi Bilioni 68.7 katika Baraza Maalum la Madiwani lililofanyika katika Ukumbi wa Manispaa ya Kibaha.


Akizungumza wakati wa kupitisha bajeti hiyo, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Mawazo Nicas, amesema bajeti hiyo ni chachu ya maendeleo kwa wananchi na imezingatia mahitaji halisi ya Halmashauri.


“Bajeti hii imepitia kamati zote, imejadiliwa na kuboreshwa. Ni wajibu wetu kuipitisha ili ikalete maendeleo kwa wananchi wetu,” amesema Dkt. Nicas.


Diwani wa Kata ya Kibaha, Omary Bula, amesema bajeti hiyo imeandaliwa kwa ushirikishwaji wa madiwani wote na kuwataka wajumbe kuipitisha kwa maslahi ya wananchi.


Awali akiwasilisha rasimu ya bajeti hiyo, Naibu Meya wa Manispaa ya Kibaha, Aziza Mruma, amesema Halmashauri imekisia kutumia kiasi hicho cha Shilingi Bilioni 68.7, ikiwa ni ongezeko la asilimia sita ukilinganisha na bajeti ya mwaka 2025/2026.


Kwa mujibu wa Mruma, katika mchanganuo wa bajeti hiyo, mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa Shilingi Bilioni 17.8, miradi ya maendeleo Shilingi Bilioni 8.7, huku asilimia 60 ya mapato ya ndani ikielekezwa kwenye miradi ya maendeleo na asilimia 40 kwenye matumizi ya kawaida.


Aidha, Shilingi Bilioni 1.4 zimetengwa kwa ajili ya mikopo ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.


Katika mwaka huo wa fedha, Halmashauri inatarajia kujenga kituo kimoja cha afya na zahanati mbili, pamoja na kutekeleza miradi ya kimkakati yenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.3. Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa maegesho ya malori yenye thamani ya Shilingi Milioni 242.3, kituo cha kibiashara Mbonde, na ujenzi wa kiwanda cha kusindika nyama chenye thamani ya Shilingi Milioni 524.7.


Baada ya majadiliano, madiwani kwa pamoja waliipitisha bajeti hiyo kwa kauli moja, wakiahidi kusimamia utekelezaji wake ili kuhakikisha inaleta tija na maendeleo kwa wananchi wa Manispaa ya Kibaha.




No comments:

Post a Comment