NA MWANDISHI WETU
WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imetoa mafunzo kwa wanafunzi Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), ili kuwajengea uelewa kuhusu namna ya kurasimisha biashara ili kupata fursa za uwekezaji na misingi sahihi ya kuanzisha na kukuza biashara.
Elimu hiyo imetolewa kwa wanafunzi hao tarehe 17 Februari, 2026 katika hafla ya ufunguzi wa klabu ya kuwezesha vijana katika masuala ya uwekezaji uliofanyika katika Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) cha jijini Dar es Salaam.
Hafla hiyo ilifunguliwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Ofisi ya Rais, Dkt. Fredy Msemwa ambapo aliwahimiza vijana kuchangamkia fursa za uwekezaji kwa maarifa na uthubutu, akisisitiza umuhimu wa kutambua tofauti kati ya Mfanyabiashara, Mwekezaji na Mjasiriamali ili waweze kufanya maamuzi sahihi katika safari yao ya kiuchumi.
Aidha, mada kuhusu usajili wa Majina ya Biashara, usajili wa Kampuni na upatikanaji wa Leseni za Biashara Kundi A, ziliwasilishwa, ambapo hatua muhimu za kufuata wakati wa kurasimisha biashara zilielezwa na Afisa Usajili Mwandamizi Bw. Englibert Barnabas.
Vile vile, Bw. Andrew Malesi aliwasilisha mada kuhusu usajili wa Alama za Biashara na Huduma pamoja na umuhimu wa kuzipa ulinzi Hataza katika kulinda ubunifu, chapa na mawazo ya kibiashara dhidi ya wizi au matumizi yasiyo halali.
Mafunzo hayo ya urasimishaji wa biashara ni sehemu ya mkakati wa BRELA wa kuwajengea vijana uelewa wa masuala ya biashara na haki miliki wakiwa bado vyuoni, ili kuandaa kizazi cha wafanyabiashara wanaofuata sheria, wenye ubunifu na wanaochangia kikamilifu katika ukuaji wa uchumi wa taifa hatua inayodhihirisha dhamira ya pamoja ya kuwawezesha vijana kuwa wawekezaji na wajasiriamali wenye mafanikio.








No comments:
Post a Comment