VIJANA WATAKIWA KUCHANGAMKIA TSH. TRIL 5 ZA MOKOPO - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Thursday, February 5, 2026

VIJANA WATAKIWA KUCHANGAMKIA TSH. TRIL 5 ZA MOKOPO


NA MWANDISHI WETU

CHAMA cha Wasambazaji wa Bidhaa na Watoa Huduma Migodini (TAMISA) kimewataka vijana na Watanzania kwa ujumla kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta ya madini kwa kutumia mikopo yenye thamani ya shilingi trilioni tano inayotolewa na Serikali kwa ajili ya kuwawezesha kupata mitaji ya kusambaza bidhaa na kutoa huduma mbalimbali migodini.


Rai hiyo imetolewa jana jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa TAMISA,  Peter Kumalilwa, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu fursa lukuki zinazopatikana katika sekta ya madini, akisisitiza umuhimu wa Watanzania kuzitumia kikamilifu kwa maendeleo yao na taifa kwa ujumla.


Kumalilwa alisema katika jitihada za kuongeza ajira na kukuza uchumi kupitia sekta ya madini, Serikali imetenga kiasi cha shilingi trilioni tano kwa ajili ya kuwawezesha Watanzania wanaojihusisha na shughuli za usambazaji wa bidhaa na utoaji wa huduma katika migodi mbalimbali nchini.


Alifafanua kuwa sekta ya madini kwa sasa inachangia zaidi ya asilimia 10 ya Pato la Taifa (GDP), huku Serikali ikitangaza fursa 20 maalum kwa wazawa kwa lengo la kuwasaidia kuhama kutoka kwenye usambazaji wa bidhaa na kuelekea kwenye uzalishaji wa bidhaa hizo.


Baadhi ya fursa hizo ni pamoja na utengenezaji wa vifaa vya ujenzi kama saruji, nondo na nyaya, uzalishaji wa vilainishi mbalimbali, utengenezaji wa vilipuzi vya miamba, huduma za kisheria pamoja na huduma za usafirishaji wa mizigo na shehena.


Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa TAMISA, Japhet Mussa, alisema Serikali inatambua dhamira ya dhati ya Watanzania wengi ya kushiriki kikamilifu katika biashara ya madini na iko tayari kuunga mkono jitihada hizo ili kuongeza ushiriki wa wazawa katika mnyororo wa thamani wa sekta hiyo.

No comments:

Post a Comment