CUF YAMPONGEZA JK - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Thursday, March 26, 2026

CUF YAMPONGEZA JK

 


Chama cha Wananchi (CUF) kimetoa salamu za pongezi kwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete, kufuatia uteuzi wake kuwa Mwakilishi wa Ngazi ya Juu wa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC) katika eneo la Pembe ya Afrika na Bahari ya Shamu.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mambo ya Nje, Bunge, Sera na Utafiti ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma wa CUF Taifa, Eng. Mohamed Ngulangwa mapema leo 26 Machi 2026 imesema uteuzi huo uliofanywa na Mwenyekiti wa AUC, Mahmoud Ali Youssouf, umetajwa kuwa ni heshima kubwa si tu kwa Kikwete bali pia kwa Taifa la Tanzania kwa ujumla.

CUF imeeleza kuwa katika kipindi chake cha uongozi, Kikwete alionyesha jitihada za kuruhusu na kukuza demokrasia ya vyama vingi nchini, japokuwa kwa kiwango cha wastani. Chama hicho kimebainisha kuwa wakati wa utawala wake, kulikuwepo na kiwango fulani cha kuheshimu kura za wananchi, hasa katika chaguzi za ubunge, udiwani na serikali za mitaa.

Aidha, chama hicho kimesisitiza kuwa Kikwete alikuwa na msimamo wa kukubali kukosolewa na kuamini katika mjadala wa hoja, jambo lililochangia kuimarika kwa ufanisi wa Bunge na kuwezesha mijadala ya wazi kuhusu masuala mbalimbali ya kitaifa, ikiwemo changamoto zilizokuwepo serikalini.

Katika taarifa hiyo, CUF pia imekumbusha kuwa ni katika kipindi cha uongozi wa Kikwete ambapo kulianzishwa mchakato wa Katiba Mpya uliolenga kukusanya maoni ya wananchi, ingawa mchakato huo haukukamilika.

Kutokana na rekodi hiyo ya uongozi, CUF imeeleza imani yake kuwa Kikwete ataitumikia vyema nafasi hiyo mpya katika Umoja wa Afrika. Chama hicho pia kimemtakia mafanikio katika majukumu yake mapya, huku kikisisitiza umuhimu wa kuendeleza misingi ya utawala bora na demokrasia nchini Tanzania.

No comments:

Post a Comment