DCEA YAKAMATA TANI 9.93 ZA DAWA ZA KULEVYA - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Wednesday, March 4, 2026

DCEA YAKAMATA TANI 9.93 ZA DAWA ZA KULEVYA

 


NA MWANDISHI WETU


MAMLAKA  ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imefanikiwa kukamata tani 9.93 za dawa za kulevya na chupa 1,795 za dawa tiba mbalimbali katika operesheni za Januari na Februari 2026. 


Operesheni hizo zilipelekea kukamatwa kwa watuhumiwa 151, magari 6, na pikipiki 29, huku ekari 87.5 za mashamba ya bangi zikiteketezwa nchini kote.  


Katika kituo cha forodha cha Mutukula, maofisa walikamata shehena ya dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya Pethidine, Morphine, na Fentanyl zilizokuwa zimesafirishwa kwenye basi la abiria la SR Classic likitokea Uganda. 


Watuhumiwa saba walikamatwa kuhusika na tukio hilo, akiwemo Hassan Omary Mwambashi (Macheni) na Ibrahim Saidi Malindi.  


Aidha, kiasi kikubwa cha bangi aina ya skanka kimeendelea kukamatwa, ikiwemo kilogramu 81.883 zilizokutwa kwenye lori la apples jijini Dar es Salaam na kilogramu nyingine 488.64 eneo la Chanika Buyuni. 


Operesheni nyingine mkoani Mbeya na Arusha zilipelekea kukamatwa kwa wasafirishaji wengine wa skanka na mirungi.  


Mamlaka imesisitiza kuwa dawa tiba hizo (opioids) ni hatari zikitumiwa kinyume na utaratibu kwani zinaweza kusababisha uraibu na vifo kwa haraka. 


Serikali imeahidi kuendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na jamii ili kudhibiti mianya yote ya uchepushaji wa dawa hizi na kutokomeza biashara haramu ya dawa za kulevya.

No comments:

Post a Comment