DKT. GWAJIMA AIPONGEZA BRELA KUSOGEZA HUDUMA ZA USAJILI KWA WANANCHI - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Sunday, March 1, 2026

DKT. GWAJIMA AIPONGEZA BRELA KUSOGEZA HUDUMA ZA USAJILI KWA WANANCHI


NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Makundi Maalumu Dkt. Dorothy Gwajima ameipongeza Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kwa kusogeza huduma za usajili wa biashara kwenye Maonyesho ya Sita ya Bidhaa za Viwanda na Biashara za Wanawake Tanzania yanayoendelea katika viwanja vya Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam. 


Akizungumza wakati alipotembelea banda la BRELA katika maonyesho hayo, leo tarehe 01 Machi, 2026, Dkt. Gwajima alisema Wakala imekuwa ikifanya kazi nzuri ya kuwasaidia wananchi kusajili biashara na kampuni zao ili waweze kufanya biashara kwenye mfumo ulio rasmi.


“Mimi ni mdau wa BRELA walinisaidia kusajili biashara yangu, ninawapongeza mnafanya kazi nzuri, endeleeni kuwasaidia wananchi kuwa rasmi katika biashara hasa wa vijijini na mimi nitakuwa balozi mzuri wa kufikisha elimu kwa wananchi wangu” alisema Dkt. Gwajima.


Awali, akieleza mkakati wa BRELA katika kuwafikia wadau wake, Msaidizi wa Msajili Mkuu wa BRELA, Bi. Hellen Mhina, alisema wakala huo unaendelea kutumia majukwaa mbalimbali ikiwemo maonyesho ya kibiashara ili kutoa elimu kwa wananchi na kuwasaidia kutatua changamoto zinazowakabili katika masuala ya usajili wa biashara na makampuni.


Waziri, tumeanza kutoa huduma katika maonyesho haya tangu tarehe 26 Februari, 2026, ambapo tumekuwa tukiwasaidia wafanyabiashara wenye changamoto za usajili wa biashara na kampuni yao, pamoja na kutoa elimu kuhusu urasimishaji wa biashara na umiliki manufaa. Tutaendelea kutoa huduma hadi siku ya kufungwa kwa maonyesho,” alisema Bi. Mhina.


Maonyesho hayo ya siku tano, yaliyoanza tarehe 26 Februari, 2026 na kushirikisha wafanyabiashara wa bidhaa za viwanda na biashara za wanawake Tanzania, yanatarajiwa kufungwa rasmi tarehe 02 Machi 2026.




No comments:

Post a Comment