TANESCO YATOA UFAFANUZI KUHUSU MALALAMIKO YA WATEJA YALIYOWASILISHWA JAMII FORUMS - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Friday, June 19, 2026

TANESCO YATOA UFAFANUZI KUHUSU MALALAMIKO YA WATEJA YALIYOWASILISHWA JAMII FORUMS

 


Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limetoa ufafanuzi kuhusu changamoto mbalimbali za upatikanaji wa huduma ya umeme zilizowasilishwa na wateja kupitia jukwaa la Jamii Forums katika maeneo tofauti nchini.


Katika taarifa yake, TANESCO imesema imefanyia kazi malalamiko hayo kwa kuyafuatilia na kuyachambua ili kubaini hali halisi na hatua zinazochukuliwa kutatua changamoto hizo.

Kuhusu malalamiko ya kukatika mara kwa mara kwa umeme katika eneo la Buswelu Center jijini Mwanza, TANESCO imeeleza kuwa tatizo husika lipo katika eneo la Buswelu Bulola na linahusiana na upungufu wa nguvu ya umeme (Low Voltage).


Shirika hilo limesema tayari limeanza utekelezaji wa mradi wa kuboresha miundombinu ya umeme katika eneo hilo kuanzia Juni 18, 2026, kwa lengo la kuimarisha upatikanaji na ubora wa huduma ya umeme. TANESCO imewaomba wananchi kuwa na uvumilivu wakati kazi hizo zikiendelea.


Kwa upande wa Kata ya Moshono jijini Arusha, ambapo baadhi ya wananchi walidai kucheleweshewa kuunganishiwa umeme kwa madai ya ukosefu wa nguzo, TANESCO imefafanua kuwa vifaa vyote vinavyohitajika kwa ajili ya kuunganisha huduma ya umeme vinapatikana na zoezi la kuwaunganishia wateja linaendelea katika maeneo yote ya Mkoa wa Arusha.


Aidha, TANESCO imezungumzia malalamiko kutoka eneo la Viwandani Manispaa ya Iringa kuhusu kukatika kwa umeme nyakati za jioni. Shirika hilo limeeleza kuwa hali hiyo haitokei kila siku bali husababishwa na changamoto za kiufundi zinazojitokeza kwenye miundombinu ya usambazaji wa umeme.


TANESCO imeongeza kuwa imekuwa ikitoa taarifa kwa wateja kila inapofanya matengenezo yaliyopangwa au pale zinapotokea hitilafu za dharura zinazoathiri upatikanaji wa huduma.


Katika Mkoa wa Tanga, TANESCO imejibu malalamiko ya wananchi wa eneo la Msambiazi wilayani Korogwe waliodai kusubiri kwa miaka mitatu kufungiwa transfoma mpya. Shirika hilo limesema tathmini ya mahitaji ya eneo hilo imekamilika na maandalizi yote ya utekelezaji wa mradi yameshafanyika.


Kwa mujibu wa TANESCO, kazi ya ujenzi wa mradi wa kuimarisha huduma ya umeme kwa kufunga transfoma mpya katika eneo hilo inatarajiwa kuanza rasmi Juni 22, 2026.


Shirika hilo limewahakikishia wateja wake kuwa linaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha huduma ya umeme nchini na kushughulikia changamoto zinazojitokeza kwa wakati.




No comments:

Post a Comment