MGONGANO WA MASLAHI WATAJWA KURUDISHA NYUMA MAENDELEO - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Sunday, June 14, 2026

MGONGANO WA MASLAHI WATAJWA KURUDISHA NYUMA MAENDELEO

 


NA MWANDISHI WETU, ARUSHA

Mgongano wa maslahi kwa watumishi wa umma umetajwa kuathiri ufanisi kwenye utendaji na majukumu ya Serikali kutokana na matokeo hasi ya vitendo hivyo vinavyopelekea kuchochea mazingira ya rushwa na kujinufaisha binafsi badala ya ofisi na kukwamisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi. 


Hayo yameelezwa mapema mwishoni mwa wiki Jijini Arusha na Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Bi. Stella Mwaiswaga wakati akifunga mafunzo kwa wajumbe wa Kamati Maalum ya Menejimenti ya ofisi hiyo yaliyolenga kuwajengea uwezo wajumbe hao katika kusimamia masuala ya uadilifu sehemu za kazi .


Aliongezea kuwa ni muhimu kuendelea kuzingatia taratibu, kanuni na sheria za utumishi wa umma ili kuepuka vitendo vinavyoathiri utendaji wa watumishi hasa katika kujali maslahi binafsi yanayochochea kukosekana kwa huduma bora kwa wananchi.


Alisema kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu imeendelea kuwa Ofisi ya mfano katika masuala ya Uratibu wa Shughuli za Serikali hivyo ni wajibu wa kila mtumishi kuendelea kuzingatia masuala ya uadilifu ikiwemo la kujilinda na vitendo vyote vinavyoweza kuharibu taswira ya ofisi hiyo.


Akiwasilisha mada kuhusu masuala ya dhana ya Mgongano wa Maslahi, Katibu Msaidizi Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Kaskazini Bw. Gerald Mwaitebele amesema ni vyema kuzingatia na kuepuka masuala ya mgongano wa maslahi katika maeneo ya kazi kwani yameendelea kuwa chachu ya kuondoa ufanisi na uwazi wa ofisi zetu.


Aliongezea kuwa,kiongozi anayetekeleza majukumu kwa kujali maslahi binafsi humpelekea kutokuwa na maamuzi sahihi na kusababisha kuharibu utendaji wa taasisi na ofisi anayoihudumia hivyo kuondoa uaminifu kwa jamii, hadi ngazi ya Taifa. 


"Mgongano wa maslahi hutokea pale ambapo maslahi yako binafsi (kifedha, kijamii au kindugu) yanapokinzana na majukumu yako ya kikazi. Hali hii inapaswa kuepukwa kwani inaharibu uadilifu, inasababisha upendeleo, na inaweza kuondoa uaminifu wa umma au wa taasisi tunazofanyia kazi," alisisitiza Mwaitebele


Akitoa neno la shukran kwa niaba ya wajumbe wa kamati hiyo, Bi.Ngole Keya, Naibu Katibu wa Mheshimiwa Waziri Mkuu ameshukuru mafunzo hayo yenye lengo la kuwajengea uelewa na kuendelea kuwakumbusha masuala ya msingi katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku.


“Kipekee tunawapongeza watoa mada wametujenga na kutupa maarifa zaidi katika kuendelea kuboresha utendaji wetu ili kuendelea kutoa huduma bora na kuhakikisha tunaendelea vyema na majukumu yetu ikiwemo la kuratibu shughuli za Serikali kwa kuzingatia misingi na kanuni za kiutumishi zinavyoelekeza,” alisema Bi.Ngole.







No comments:

Post a Comment